UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA USITUGAWANYE- DKT. BITEKO



UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA USITUGAWANYE- DKT. BITEKO

Na,Mwandishi wetu-Bukombe Geita

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu nchini, usiwe kigezo cha kugawa wananchi bali watu wote waungane, wapendane na wathaminiane ili kuendelea kudumisha amani iliyopo.

Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo leo tarehe 1 Januar, 2024 wakati alipojumuika na wananchi wa Bukombe katika sherehe za kuukaribisha mwaka 2024 nyumbani kwake kitongoji cha Bulangwa, wilayani Bukombe mkoani Geita ambapo ametoa pia salam za mwaka mpya.

"Mwaka huu utakuwa mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kamwe uchaguzi huu usitugawe kwa misingi ya vyama vya siasa lakini utuunganishe zaidi, watu wote tunapaswa tupendane, tuthaminiane na tushirikiane, tunazo tofauti nyingi  ikiwemo za makabila, dini na vyama vya siasa lakini kamwe visitugawanye, tuungane wote na tushikamane." Amesema Dkt. Biteko.

Kuhusu Salam za Rais, Dkt. Samia za Mwaka 2024 alizozitoa kwa watanzania, Dkt. Biteko amesema, Sekta ya Nishati itaiishi kauli ya Rais ya kuwa, mwaka 2024 utakuwa ni mwaka wa vitendo na si maneno na kwamba watafanyia kazi maelekezo yake kwa nguvu zote na ubunifu ili wananchi wapate huduma bora.

Dkt. Biteko ameshukuru wananchi wa Bukombe kwa ushirikiano wanaompa katika utekelezaji wa majukumu yake akieleza  kwamba watu wa Bukombe wamekuwa si watu wa kunung'unika bali kuboresha pale wanapoona kuna upungufu.

Akitoa salam salam za mwaka mpya 2024, Dkt. Biteko ametaka wananchi kupendana, kuthaminiana na kushirikiana  na kila mtu aazimie kumfanya mtu mmoja awe na furaha na kusameheana.

Sherehe za kukaribisha mwaka 2024 wilayani Bukombe zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, Wabunge  wa Mkoa wa Geita, Madiwani wa Kata mbalimbali wilayani Bukombe na viongozi wa Vijiji.

Huu umekuwa ni utamaduni  ambao Dkt. Doto Biteko amekuwa akiufanya kutoka mwaka 2016 wa kujumuika na wananchi katika kukaribisha mwaka mpya.

Mgeni maalum katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amempongeza Dkt. Biteko kwa utamaduni huo, ambao haubagui dini, kabila, itikadi za kisiasa au hadhi ya mtu.

Amesema utaratibu huo umewezesha wananchi kujumuika pamoja, kufurahi, kutafakari yale waliyofanikiwa na yaliyoshindwa kufanikiwa,  kuweka jitihada katika mwaka 2024 na kuweka mikakati ya nini kifanyike katika mwaka huuili Jimbo la Bukombe liweze kusonga mbele.

Post a Comment

Previous Post Next Post