UTUNZAJI MZURI WA KUMBUKUMBU NA NYARAKA UNACHANGIA KUBORESHA VYANZO VIPYA VYA UKUSANYAJI WA MAPATO KUPITIA TAARIFA ZILIZOHIFADHIWA-MHE. ABDULLA


UTUNZAJI MZURI WA KUMBUKUMBU NA NYARAKA UNACHANGIA KUBORESHA VYANZO VIPYA VYA UKUSANYAJI WA MAPATO KUPITIA TAARIFA ZILIZOHIFADHIWA-MHE. ABDULLA

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema katika kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji katika kupiga hatua za kimaendeleo unahitaji utunzaji mzuri wa kumbukumbu na nyaraka kwa maslahi ya Taifa na watu wake.

Maneno hayo ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi yametoleo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais Dkt. Husseni Ali Mwinyi  katika Mkutano wa 12 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Aidha, amesema Serikali na taasisi binafsi zinatumia kumbukumbu na Nyaraka katika kupanga, kutathmini na kufanya maamuzi kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi au Taasisi husika.

"utunzaji mzuri wa kumbukumbu na nyaraka unachangia kuboresha vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato kupitia taarifa zilizohifadhiwa na taarifa hizo zinasaidia kuonesha maeneo ya uwekezaji yakiwemo ya utalii yanayokuza pato la Taifa na kuimarisha miradi ya maendeleo". Amesema

Kadhalika,Mhe. Hemed amesema kumbukumbu na nyaraka zinaisaidia Serikali katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma na kutumika kama nyezo muhimu inayomsaidia Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kukagua na kudhibiti uhalali wa matumizi ya fedha za Umma.

"kumbukumbu na Nyaraka zinaisaidia Serikali kufahamu taarifa za watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo, wanaotarajiwa kustaafu pamoja na mambo mengine ikiwemo haki na wajibu kwa wafanyakazi". Amesema

"Nazisisitiza Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri wa kukutana na Uongozi wa TRAMPA ili kuangalia changamoto mbali mbali zinazojitokeza kwa watendaji wa kada hizo na kuzichukulia hatua stahiki kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji wao". Amesisitiza

Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema serikali itaendelea kuajiri maofisa kumbukumbu na nyaraka ili  kupunguza changamoto ya maofisa hao.

Awali akisoma Risala ya wanachama wa chama cha Menejiment ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania ( TRAMPA ) Mwenyekiti wa chama hicho  Bi. Devotha Mrope amesema Kumbukumbu na nyaraka zinapotunzwa vizuri zinaisaidia jamii na Serikali kutambua tulikotoka, tulipo na tunakoelekea.

"hivyo TRAMPA imejipanga katika kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwapa taaluma na  ujuzi watendaji wa kada hii ili kuongeza ari na ufanisi wa kazi zao". Amesema

"Nazipongeza Serikali zote mbili  kwa kuanzisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA katika Taasisi za Serikali itakayosaidia kutunza Kumbukumbu kwa ufasaha na weledi wa hali ya juu jambo ambalo litachangia kasi ya maendeleo nchini". Ameongeza

Samabamba na hayo Bi Mrope amezitaja  changamoto zinazoikabili TRAMPA ni pamoja na waajiri kuendelea kutumia karatasi katika utunzaji wa kumbukumbu na Nyaraka pamoja na uhaba wa vyumba maalum kwa ajili ya masjala za siri jambo ambalo linachangia kwa kiasi mkubwa uvujaji wa taarifa za siri katika Taasisi nyingi nchini.

"Naziomba serikali zote mbili kuweza kuzitatua changamoto hizi ili kuleta ufanisi nzuri wa kazi kwa maslahi mapana ya Taifa". Amesisitiza.





Post a Comment

Previous Post Next Post