PROF SEDOYEKA AKATAA TUHUMA NNE ZINAZOMKABILI
Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma octoba 17 imemaliza kusikiliza malalamiko dhidi ya tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA),Prof.Eliamini Sedoyeka, anayetuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi hiyo, kinyume na kanuni na taratibu za maadili ya uongozi wa umma ambapo amekana tuhuma zote.
Prof. Eliamini Sedoyeka amefikishwa kwenye Baraza la Maadili kutokana na malalamiko manne ya kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
Malalamiko hayo ni kumpandisha cheo mtumishi kwa upendeleo, kuingilia mchakato wa ununuzi wa viti na meza, kuwa na uhusiano wa karibu na mtumishi na kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi kinyume na maadili ya viongozi wa umma.
Kikao cha baraza hilo kimeketi jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Baraza Jaji Mstaafu Rose Temba na upande wa mlalamikaji umewakilishwa na Mawakili wa Serikali Emma Gellan na Hassan Mayunga.
Akisoma hati ya malalamiko mbele ya Baraza, Emma amesema kuwa Prof. Sedoyeka akiwa anatekeleza majukumu yake ya uongozi pasipo kufuata Sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma alimpandisha cheo Hakimu Ndatama kutoka Afisa Rasilimali daraja la pili na kuwa Mkuu wa Sehemu ya Rasilimaliwatu kabla ya kukamilika kwa uhamisho wa mtumishi huyo na bila kuwa na sifa na vigezo.
Pia, amesema malalamiko mengine kuwa na uhusiano wa ukaribu na Ndatama kwa kufanya naye kazi IAA na kisha Wizara ya Maliasili na Utalii na aliporudishwa tena IAA, Mtumishi huyo aliombewa ahamie IAA mara tu baada ya mlalamikiwa kuteuliwa kuongoza taasisi hiyo.
Kadhalika kuingilia mchakato wa zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza katika Kampasi ya Babati kwa kuifuta bila kufuata utaratibu na bila sababu za kisheria.
Pia, Prof.Sedoyeka anakabiliwa na malalamiko ya kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi Robert Mwitango (Afisa Ugavi) kutoka Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kwenda Idara ya Maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi.
Baada ya kusomewa tuhuma zinazomkabili mlalamikiwa Prof Eliamini Sedoyeka amekana tuhuma hizo zote nne zilizowasilishwa mbele ya baraza.
Baada ya Baraza hilo octoba 17, 2024 kukamilisha kupokea ushahidi wa pande zote mbili sasa Wajumbe wataingia katika mchakato wa kuandaa taarifa ya uchuguzi pamoja na mapendekezwa yao kisha kuwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kuhusu walichokibaini.