WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA RED EYES



WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA RED EYES

Na WAF - Dodoma.

Wizara ya afya imewaasa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa macho mekundu (Red eyes) Maambukizi ya Kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” iliyoibuka  nchini hivi karibuni.

Hayo yamesemwa leo Januari 15, 2023 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa awali ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kuathiri watu wengi nchini.

Prof. Ruggajo amesema dalili ya ugonjwa huo ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi na kutoa tongo tongo za njano.

"Taarifa za uchunguzi zinaonesha Maambukizi ya Kirusi hiki kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa. Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili". Amesema Prof Ruggajo.

Prof. Ruggajo amesema mwenendo wa ugonjwa huo unaonyesha kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika katika Vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wanasumbuliwa na ugonjwa huo. 

“Katika kipindi cha Desembe 22, 2023 hadi Januari 11, 2024 kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya matibabu, kwa mfano katika mkoa wa Dar Es Salaam kuna wagonjwa wapya 869 huku hali ya kawaida katika kipindi cha mwezi Desemba 2023 kulikuwa na wagonjwa 17 pekee” amefafanua Prof. Ruggajo.

Aidha amesisitiza suala la usafi ni jambo muhimu katika kuzuia maambukizi kusambaa kwa wengine Kutokana na tabia ya ugonjwa huu kusambaa kwa kasi, maambukizi haya huleta mlipuko ambao husambaa kupitia kirusi kwa asilimia zaidi ya 80%.

Prof Ruggajo amewashauri wananchi kutokutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hazijaandikwa na daktari kwa wakati huo na kutotumia  dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti na kwa matumizi tofauti.

Post a Comment

Previous Post Next Post