SERIKALI IMEDHAMIRIA KUANZA UJENZI WA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA DODOMA.
N,Saleh Lujuo-Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Washauri elekezi wa Chuo Kikuu cha Hanyang cha Korea wamefungua rasmi maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha TEHAMA Dodoma eneo la Nala ambacho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 15,000 kwa mwaka huku upembuzi wake yakinifu utachukua miezi sita kukamilika.
Aidha Wizara hiyo pia imetumia nafasi hiyo kuwatangazia watumishi wa Serikali kuomba ufadhili wa masomo ya muda mrefu na muda mfupi yanayotolewa na Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya TEHAMA.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma Januari 29,2024 na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw, Mohammed Khamis Abdulla wakati akizungumza na Waandishi wa habari ambapo ameeleza kuwa mahitaji ya awali ya Chuo hicho yanajumuisha aina ya majengo na masomo yatakayo fundishwa yameandaliwa na kuwasilishwa na Exim Bank.
Amesema, Serikali imeweka mpango wa ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi wa Umma 500 kwenye kozi za kuongeza ujuzi kwenye masuala yanayohusu TEHAMA hususani Teknolojia .
"Leo hii nawatangazia Watumishi wa Umma uwepo wa nafasi 440 za ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi kwenye masuala yaTEHAMA na Teknolojia zinazoibukia kwa Watumishi wa UmmaWizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - UTUMISHI (OR-MUUUB) tutaendelea kuhakikisha tunasimamia mafunzo kwa kada hii ya TEHAMA kwa watumishi wa Umma, "amesisitiza na kuongeza". Amesisitiza
"Hivyo basi napenda kuwatangazia watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa tumefungua dirisha la maombi hayo kupitia tovuti ya www.scholarship.go.tz." Ameongeza.
Kwa upande wa timu ya Washauri elekezi inayoongozwa na Prof. Taejoon Park imesema hatua hiyo imetokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hiyo na kwamba kazi hiyo itafanywa kwa ufanisi na ujuzi mkubwa kwa kipindi cha muda wa miezi sita.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ally Gugu akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, amesema kuwepo kwa chuo hicho eneo la Nala kitaleta mchango mkubwa katika Masuala ya TEHAMA nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Prof, Lugano Kusiluka,amesema ujenzi huo utakapo kamilika utasaidia Kwa kiasi kikubwa kuwainua vijana na kujiletea maendeleo yao.
"Kwa kuwa na Sisi tuna ndaki ya TEHAMA tutashirikiana bega kwa bega kufanikisha maono ya Serikali kuwatayarisha wataalamu watakaofundisha chuo hiki kinachoanza kujengwa na tayari tumetenga jengo kwa ajili ya jambo hili kuwapika vijana kutafsiri maono ya Rais Samia, lengo ni kuongeza uwekezaji unaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia Duniani, "amesema.
Utekelezaji wa Miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2021-2026 na ilani ya chama cha mapinduzi ccm ya mwaka 2020-2025 ambayo inasisitiza uwepo wa mafunzo ya ujuzi na ubunifu katika TEHAMA nchini.