VIFO VINGI DUNIANI KOTE HUTOKANA NA MAGONJWA YANAYOTOKEA KWA WANYAMA KWENDA KWA BINADAMU-MHE. MHAGAMA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Inakadiriwa kuwa, duniani kote, takriban visa bilioni moja vya ugonjwa na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Aidha, ni Asilimia 60 ya magonjwa ya kuambukiza yanayoibuka ambayo yanaripotiwa ulimwenguni kote ni magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Takwimu hizo amezitoa Waziri wa nchi Ofisi ya waziri mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama jijini Dodoma katika Ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Afya Moja ambapo amesema kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayoibuka kutokana na mwingiliano uliopo baina ya binadamu, wanyama na mazingira.
Na hii inatokana na mwingiliano mkubwa wa shughuli za kijamii na kiuchumi, mwenendo na mifumo ya maisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
"zaidi ya 75% ya vimelea vipya vya magonjwa vilivyogunduliwa katika miongo mitatu iliyopita, 30% vimetoka kwa wanyama". Amesema
"Changamoto hii ni kubwa na inahitaji ushirikiano wa kisekta ili kudhibiti magonjwa haya na matukio mengine yenye athari mtambuka kwa kutumia mbinu ya Afya Moja". Ameongeza
Aidha,waziri Mhagama amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu imeendelea kuimarisha mifumo ya utendaji ya usimamizi wa maafa yanayoathiri afya ya binadamu, wanyama, mimea na mifumo ya ikolojia kupitia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Mwaka 2004 ambayo imeweka kipaumbele udhibiti wa magonjwa ya milipuko ili kuzuia maafa yanayoweza kutokea.
"Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na.6 ya Mwaka 2022 inabainisha majukumu ya kutekelezwa kwa kuzingatia ushirikiano wa wadau kwa dhana ya afya moja. Vilevile, Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa 2022 – 2027 umeanisha umuhimu wa kutekeleza hatua za kuimarisha uwezo wa kutumia dhana ya afya moja kwa maafa yanayohusiana na masuala ya afya katika ngazi zote kwa ustahimilivu wa jamii". Amesema.
"Dhana hii ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya sekta zinazohusika na afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa ajili ya uratibu na usimamizi katika utendaji na kupanga mikakati ya pamoja inayolenga kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea na mazao ikiwemo madhara ya majanga yanayovuka mipaka na yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza". Ameongeza.
Sambamba na hayo waziri Mhagama amesema Serikali inaendelea kuongeza uelewa kuhusu dhana ya Afya Moja na umuhimu wake ambapo ametoa wito kwa wadau wote kuungana na Serikali kuendelea kutoa elimu hasa katika ngazi ya jamii ili iweze kujilinda na magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
"nitoe rai kwa Wizara, Idara na Taasisi za Umma, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kuendelea kuimarisha utekelezaji wa masuala ya usimamizi wa dharura katika maeneo yao ili kuhakikisha shughuli zote za maendeleo zinakuwa stahimilivu kwa maslahi mapana na Nchi yetu". Amesisitiza.
"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuzingatia na kusimamia Sera, Sheria na Mikakati kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisekta katika kupambana na magonjwa ya milipuko na matukio yanayoathiri binadamu, wanyama na mazingira". Ameongeza
Vile vile Mhe. Mhagama amesema, utendaji wa pamoja kwa dhana ya Afya Moja imekuwa ni nyenzo ya kuimarisha usalama wa chakula na lishe na kupunguza madhara ya magonjwa yasiyoambukiza na usugu wa madawa.
"Serikali inaendelea kuzingatia umuhimu kwa wataalamu wa sekta mbalimbali kuongeza ushirikiano na mawasilaino katika nyanja za afya ya binadamu, wanyama na mazinigira". Amesema
"Mfumo wa uratibu na utendaji wa pamoja ni silaha muhimu katika kuwezesha wataalam kuchukua hatua kwa muda mfupi na matumizi ya rasilimali kidogo". Amesisitiza
kaulimbiu ya kongamano hilo ni:“Afya Moja: Mbinu ya Pamoja kuboresha afya ya binadamu, wanyama, mimea na mfumo wa ikolojia kwa ustahimilivu wa maafa.”.