TANZANIA NA MAREKANI KUSHIRIKIANA KUFANYA UTAFITI WA MADINI KINYWE NCHINI


💧Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi,Tanzania na Marekani zimeonyesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu ambapo  kupitia wizara ya Madini na Nishati ya Marekani wanaenda kutekeleza utafiti wa Madini Kinywe hapa nchini, hatua inayolenga kubaini maeneo yenye madini hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde leo January 26,2026 Jijini Dodoma  alipokutana na  Wizara ya Madini na Nishati ya Marekani ambapo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani unalenga kutumia teknolojia ya kisasa katika utafiti wa madini, kubaini rasilimali zilizopo, na kufanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini yenye mahitaji makubwa duniani.

Tunaishukuru Marekani kwa kuendelea kushirikiana nasi katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi, ikiwemo kupitia rasilimali na sekta muhimu za uzalishaji,” amesema Waziri Mavunde.

Kadhalika,Waziri Mavunde Ameongeza kuwa kupitia Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati ya Marekani, zimeandaliwa programu maalum zitakazosaidia utekelezaji wa ajenda za maendeleo, hususan katika kuendeleza sekta ya madini na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani.

“Tanzania inafahamika kimataifa kwa kuwa na madini yenye mahitaji makubwa, hali inayofanya ushirikiano huu kuwa fursa muhimu ya kujenga uwezo wa Watanzania, hususan katika utafiti wa kisasa wa kijiolojia,” ameongeza.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, amesema ushirikiano huu ni kielelezo cha uhusiano thabiti kati ya pande zote mbili katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia.

Utafiti huo unalenga kuisaidia Serikali ya Tanzania kupata takwimu sahihi za rasilimali zilizopo, hususan katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambako dalili za uwepo wa Madini ya Kinywe tayari zimeshapatikana, huku mipango ikiwa ni kupanua zaidi eneo la utafiti.

Post a Comment

Previous Post Next Post