💧SERIKALI kupitia wizara ya viwanda na Biashara imeweka mkazo mpya katika kuleta viwanda karibu na wananchi kupitia mitaa ya viwanda na kongani kwa lengo la kufungua milango Kwa vijana kumiliki na kuendesha viwanda na Biashara zao ili kujipatia kipato.
Kauli hiyo ameitoa waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga leo January 24,2026 Jijini Dodoma wakati akieleza ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani katika kipindi Cha siku mia Moja za uongozi wake baada ya uchaguzi Mkuu.
Amesema utekelezaji huo wa uendelezaji wa mitaa ya viwanda na programu ya vijana kipato cha wakulima kinaongezeka kupitia uongezaji thamani, na maelfu ya vijana wanafunguliwa milango ya kumiliki na kuendesha viwanda na biashara ndani ya kongani hizo.
"Tathmini ya awali ya kongani na mitaa ya viwanda imekamilika katika mikoa 11 nchini ikibainisha mahitaji ya wajasiriamali na maeneo yenye uwezo mkubwa wa uongezaji thamani wa mazao". Amesema
Aidha,waziri Kapinga amesema serikali imekamilisha mchakato wa kufunga Kiwanda cha kuchakata zao la Muhogo mbichi kupata unga wa muhogo katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Tanga.
"Kufungwa Kwa mtambo huu kutawezesha kukausha tani kumi na mbili (12) za muhogo mbichi kwa saa kumi (10) na kutoa tani 3 za unga wa muhogo". Amesema
"Mradi unatoa ajira 150 za moja kwa moja na zaidi ya ajira 300 zisizo za moja kwa moja kwa vijana na akina mama wazalishaji wa zao la muhogo". Ameongeza
Kadhalika,Waziri Kapinga amesema katika kuimarisha na kuvikuza viwanda hapa nchini serikali imeshaanza mchakato wa Kuainisha maeneo yenye madini muhimu ya kimkakati (critical minerals) nchini, ikiwemo yale yanayohitajika katika viwanda vya teknolojia, nishati jadidifu na magari ya umeme.
" utafiti huu wa kina wa madini muhimu tumeanza na Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera,Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida". Amesema
" na tutafanya kazi za uhamasishaji na ushirikishaji wa jamii katika maeneo husika kuhusu uchimbaji salama, ulinzi wa mazingira, afya na fursa za biashara ndogo zinazotokana na shughuli za utafiti na uchimbaji". Amesisitiza
Katika kudumisha na kuimarisha amani ya nchi, Msemaji mkuu wa serikali na katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amewaasa vijana kote nchini kuwa mstari wa mbele kuilinda na kuidumisha Amani iliyopo nchini.
"Serikali imeshaweka Miundombinu Rafiki kwenu vijana,hivyo mnapaswa Kulinda Amani hii tuliyonayo". Amesema
Sekta ya Viwanda na Biashara imeonesha mwelekeo thabiti na wa matumaini katika mambo makuu Mbalimbali ikiwemo Mikopo 193 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 820 imetolewa na kuzalisha ajira 546 nyingi kwa vijana.


