TBS YATOA VYETI NA LESENI ZA UBORA 2,402, WAJASIRIAMALI WADOGO WAKIWA 1,066.

TBS YATOA VYETI NA LESENI ZA UBORA 2,402, WAJASIRIAMALI WADOGO WAKIWA 1,066.

Na Deborah Lemmubi-Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt Ashura Katunzi ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita jumla ya vyeti na leseni za ubora 2,402 vimetolewa kwa wazalishaji wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,066.

Dkt Katunzi ameyasema hayo leo Jijini Dodoma Machi 18,2025 akizungumza na Wanahabari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Shirika hilo ndani ya miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. 

Na kuongeza kuwa Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya Shilingi milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila malipo yeyote.

"Aidha, jumla ya vyeti na leseni za ubora 2,402 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,066. Serikali kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya sh. milioni 350 kila mwaka kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote".

" Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na pia kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa". 

Aidha amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Shirika limeendelea na huduma za usajili wa maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya maeneo 31,592 yalisajiliwa.

Dkt Katunzi amesema kuwa katika kuhakiki ubora wa bidhaa kwa magari yaliyotumika kabla ya kuingia nchini kutoka nje ya nchi, jumla ya shehena za bidhaa 18,588 zilikaguliwa sanajari na magari 162,160 wanafanya hivi kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja kulinda afya ya warumiaji.

 "Pia, katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini ambapo kwa kipindi cha miaka minne, jumla ya shehena za bidhaa 18,588 zilikaguliwa, sanjari na magari 162,160".

"Bidhaa hizi zinakaguliwa kwa lengo la kuiepusha Tanzania kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji".

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya sekta za Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa na linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango Sura 130.

Post a Comment

Previous Post Next Post