SERIKALI IMEJIPANGA KUPUNGUZA UHABA WA WATAALAMU WA TEHAMA NCHINI-SILAA


SERIKALI IMEJIPANGA KUPUNGUZA UHABA WA WATAALAMU WA TEHAMA NCHINI-SILAA

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Katika kuchochea ukuaji wa Sekta ya TEHAMA nchini,serikali imedhamiria kupunguza uhaba wa wataalamu wa TEHAMA hasa katika teknolojia zinazochipukia na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utaalamu na uvumbuzi wa kidigitali.

Kauli hiyo ya serikali ameisema waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa leo Disemba 5,2024 jijini Dodoma ambapo amesema serikali imedhamiria kujenga Chuo mahiri cha TEHAMA (DTI) katika eneo la Nala mkoani Dodoma ili kuendelea kukuza bunifu za Watanzania. 

Aidha, waziri Silaa amesema chuo hicho pia kitasaidia kuimarisha mafunzo ya ujuzi na ubunifu katika TEHAMA.

"Chuo hiki Cha TEHAMA kitakuwa kituo muhimu sana katika kuboresha  Bunifu mbalimbali zinazozalishwa na watanzania wenyewe na kitakuwa na kazi ya kuwachukua vijana wale wenye bunifu zao walioko mtaani kuweza kuwasaidia bunifu zao kuwa tija na kufuata sheria". Amesema

"kwa mfano unakuta kijana anafanya ubunifu kumbe ule ubunifu wake ni kinyume cha sheria lakini kwa akili yake anaona ule ubunifu uko vizuri,sasa hatua hii itaweza kuwasaidia pakubwa wabunifu wetu". Ameongeza

Kadhalika waziri Silaa, amesema kazi nyingine ya chuo hicho itakuwa ni kuwaunganisha wadau mbalimbali na zile bunifu ili wapate sehemu ya kufanyia majaribio na ikitoka pale iwe bidhaa inayouzika pamoja na taasisi kubwa za ndani na nje ya nchi zinazohitaji bunifu hizo zipate sehemu ya kufikia.

Samabamba na hayo amesema zipo hatua ambazo tayari zimeshafanyika kuelekea ujenzi wa Chuo hicho ikiwemo upembuzi yakinifu ambapo ujenzi huo utakamilika ndani ya miaka miwili. 

Mwezi Septemba Serikali ilipokea taarifa ya mwisho ya upembuzi yakinifu wa ujenzi Chuo Mahiri cha TEHAMA (Digital Technology Institute - DTI) katika eneo la NALA, Dodoma kutoka kwa Mshauri elekezi kutoka Muungano wa Chuo Kikuu cha Hanyang kinachojumuisha Chuo Kikuu cha Hanyang, Kampuni za Uhandisi na Usanifu Majengo za Yooil Engineering & Architects, na Moon Engineering.

Post a Comment

Previous Post Next Post