WATANZANIA JENGENI UTAMADUNI WA KUSHIRIKI MAONESHO YA NANENANE ILI MPATE ELIMU MBALIMBALI KUHUSU KILIMO-NDERIANANGA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga ametoa Wito kwa Watanzania wa Kanda ya Kati na Mikoa mingine ya jirani kutembelea Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya NANENANE ili kuweza kujifunza teknolojia mpya na ubunifu mbalimbali.
Mhe. Ummy ametoa wito huo leo tarehe 04 Agosti, 2024 wakati alipotembelea Maonesho hayo ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea katika Uwanja wa Nzuguni Jijini Dodoma.
Aidha, Naibu Waziri Ummy amesema kuwa, amefurahishwa na maonesho hayo yaliyowavuta wananchi mbalimbali ikiwemo watu wenye walemavu.
“Nimevutiwa kuona kuwa fursa hii ya nanenane imewavuta pia wenzangu watu wenye ulemavu wamekuja kuonesha shughuli zao ambazo wanazifanya hivyo nitoe wito kwa Watanzania kutembelea Maonesho hayo ili wajifunze teknolojia mpya” amebainisha Mhe. Ummy.
Vilevile Mhe. Ummy ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga eneo hilo na kulifanya kuwa bora na la kisasa hivyo kuhamasisha wananchi kutembelea Maonesho hayo na kuona kazi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya sita.
Katika maeonesho hayo, Mhe. Ummy ameambatana na viongozi wengine wa jiji la Dodoma akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mkuu wa Wilaya ya Bahi na Wakurugenzi ambapo wametembelea mabanda mbalimbali ikiwemo banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu, Banda la Wizara ya Kilimo, banda ya sekta binafsi, DUWASA, vitalu, pamoja na banda ya wadhamini wa maonesho hayo.
Kitaifa Maonesho hayo yanaendelea Kanda ya Kati katika Uwanja wa Nzuguni Jijini Dodoma na yamebeba Kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo”