BRELA IMEDHAMIRIA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA WAKULIMA NCHINI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Kutokana na serikali Kuendelea kuwahimiza wakulima kutumia Teknolojia za kisasa Kwenye kilimo ili kuongeza Tija,Wakala ya usajili wa biashara na leseni(BRELA) imekuja na mpango wa kuanza kuwasajili wakulima ili nao wawe na nembo za biashara kupitia mazao yao.
Hayo yamebainishwa na Afisa usajili wa BRELA Gabriel Gilangay katika viwanja vya nanenane Nzuguni Jijini Dodoma ambapo amesema wakala hiyo itawasaidia wakulima kusajili Biashara zao ili kuwa na usajili wa kampuni, ushirika au Biashara ndogo ndogo zinazohusiana na kilimo.
Aidha,amesema kama Wakala watahakikisha wanawasaidia wakulima ambao wanalima kibiashara kwa kuwasajili kwa utambulisho wa lebo maalum ambazo zitawasaidia kufanya kazi zao.
" Kwa kufanya haya ni kuhakikisha kila mkulima anapata ulinzi katika suala zima la teknolojia ya bidhaa zao watakazozalisha". Amesisitiza.
"BRELA tumekuwa tukisajili biashara zikiwemo Makampuni kwakutoa leseni kwa watu wote ambao wanataka kuanzisha biashara,".Amesema
Kadhalika, Gilangay amesema wakala hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na huduma wanazozitoa ambapo mwitikio umekuwa ni mkubwa.
Dhima ya Wakala ya usajili wa biashara na leseni (BRELA) ni kuweka mazingira wezeshi ya Biashara nchini kwa kurasmisha biashara na kulinda miliki ubunifu kupitia usajili, utoaji wa leseni na udhibiti wa mwenendo wa biashara.