MAGEREZA YOTE NCHINI KUANZA KUTUMIA GESI ASILIA-MHANDISI MRAMBA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Wizara ya Nishati kupitia wakala wa nishati vijini (REA) imeingia makubaliano na magerezo yote nchini ili watumie Gesi asilia Magerezani kwa lengo la kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya nishati chafuzi inayochangia uharibifu wa mazingira.
Kauli hiyo ameitoa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba mara baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Nishati na taasisi zake kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesema Wizara ya Nishati imejipanga ipasavyo kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 - 2034) ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi ili kufikisha lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi katika kipindi cha miaka 10.
"Tunafanya kazi na taasisi zinazolisha watu wengi mfano Magereza, hivyo wizara ya Nishati kupitia REA tumeingia makubaliano na magereza zote kwamba watawekewa mitungi mikibwa pamoja na kuwekewa majiko Maalumu yanayotumia mkaa ambao hauathiri Mazingira Wala hautoi moshi na haya yote yanafanyika kwa lengo la kuachana na matumizi ya nishati chafuzi inayochangia uharibifu wa mazingira". Amesisitiza
Aidha, Mhandisi Mramba ameongeza kuwa Jitihada hizo za serikali ya awamu ya sita kwa uongozi Mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuelekea kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Kwa kushirikiana na wafanya Biashara,wabunge pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi.
'Katika Sekta ya Nishati inafungamanisha Sekta nyinginezo ikiwemo Madini, Maji, Kilimo na Mifugo ambapo katika Mifugo vinyesi vya wanyama hutumika kuzalisha nishati kwa ajili ya matumizi mbalimbali". Amesema
Serikali ya Tanzania kupitia Sera mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa inatambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi.