WIKI YA TATHMINI NA UFUATILIAJI ITUMIKE KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI WA SHUGHULI ZA SERIKALI-DKT. YONAZI
Na,Mwandishi wetu-Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza itumike katika kuongeza Ufanisi na Utendaji wa Shughuli za Serikali ili kuhakikisha kunakuwa na matokeo chanya kwa Maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha pili cha Maandalizi ya Kongamano la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza kilichofanyika tarehe 14 Mei, 2024 Jijini Dodoma.
Dkt. Yonazi ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wajumbe wa kikao hicho kutumia Makongamano hayo kwa lengo la kuonesha fursa zaidi ya kile kinachotarajiwa katika kuwavutia wawekezji nchini.
“Yatumieni makongamano haya kwa tija na mshirikishe wadau kwa lengo la kuendeleza ushirikiano na kuchochoea wawekezaji nchini, hivyo Makongamano haya yahusishe sekta za kiuchumi ikiwemo za utalii, uwekezaji pamoja na masuala ya sanaa na utamaduni ili kuchagiza mazingira bora ya biashara na uwekezaji," alisisiza Dkt. Yonazi
Kongamano hilo la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza linatarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar mwanzoni mwa mwezi Septemba, 2024