RAIS SAMIA SULUHU HASSAN ANAHITAJI KUONA KAZI NZURI NA YENYE UBORA UNAOENDANA NA FEDHA ZINAZOTOLEWA KATIKA KUTEKELEZA MIRADI-MHANDISI KASEKENYA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amewasisitiza Mafundi sanifu nchini kufanya kazi kwa uadilifu na ubora kwani Rais Samia Suluhu Hassani anahitaji kuona kazi nzuri na yenye ubora unaoendana na fedha zinazotolewa.
Akifunga Mkutano wa Sita wa Mafundi Sanifu wa Mwaka 2024 leo Mei 24,2024 Jijini Dodoma, Naibu waziri Kasemenya amesema weledi na uadilifu ni nguzo pekee itakayoisaidia Serikali kufikia azma yake ya kukuza uchumi.
"Niwasihi Mafundi sanifu katika ujenzi wa miradi mnayotekeleza miradi iendane na thamani ya fedha inayotolewa kwa kufanya kazi kwa uadilifu na ubora". amesema
Aidha, amesema Mafundi Sanifu ni kada muhimu katika maendeleo nchini katika ujenzi wa viwanda na ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Wakili Menye Manga, amesema maazimio na mapendekezo ya mkutano huo ni mafundi sanifu wasajiliwe kwa wingi ili watambulike na kuweza kupata fursa mbalimbali za maendeleo nchini.
Hata hivyo, amesema dhamira ya Mkutano huo ni kubadilishana uzoefu kupitia teknolojia mbalimbali zinazoibuka duniani kama matumizi ya akili mnemba katika Sekta mbalimbali ili kuweza kusambaza utaalam huo nchini.
Mkutano wa Sita wa Mafundi Sanifu wa Mwaka 2024 umehudhuriwa na Mafundi Sanifu 900 kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.