SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA MAFUNDI SANIFU KATIKA UKUAJI UCHUMI.



SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WA MAFUNDI SANIFU KATIKA UKUAJI UCHUMI.

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Serikali imesema inatambua mchango wa mafundi sanifu nchini katika kuufikia uchumi shindani unaokwenda sambamba na matokeo ya ubunifu na mabadiliko ya teknolojia.

Akifungua mkutano wa Sita wa Mafundi Sanifu Tanzania wa Mwaka 2024  leo Mei 23,2024, waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema Wizara ya Ujenzi inaandaa mpango wa kuwawezesha vijana kwa kuwajengea kesho iliyo bora “Building a Better Tomorrow (BBT)” katika kada ya Uhandisi, Ukandarasi na Wabunifu Majengo kwa kutenga miradi ambayo itawaongezea uzoefu katika kazi zao.

“Wizara ya Ujenzi, tumepanga kuandaa mpango unaofanana na BBT kiuhandisi katika Sekta ya Ujenzi ili tuwawezeshe vijana mnaoungana katika makundi na kuanzisha Kampuni ambapo tutawapatia miradi ya kutekeleza na tutawasimamia kwa kuzingatia taaluma zenu kwa kuwalea hadi kuwa Kampuni kubwa”, amesisitiza Bashungwa.

Hata hivyo,amewaagiza Mafundi sanifu wote nchini kuendelea kujisajili katika Bodi ya ERB kama yalivyo matakwa ya Sheria ili waweze kutambulika na kuwapa mazingira wezeshi katika fursa mbalimbali za miradi ya ujenzi inayoendelea hapa nchini ambapo amesisitiza kuwa idadi ya mafundi sanifu waliopo ni ndogo ikilinganishwa na wanaohitimu kila mwaka.

Amesema Serikali inawaamini na inatambua kuwa wapo wahandisi na mafundi sanifu wazawa ambao wanafanya kazi na wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa uadilifu na kuhakikisha viwango na ubora.

"Ni vizuri mafundi sanifu wajisajili kwa wingi ERB ili kunufaika na fursa ambazo zinatolewa na serikali na kuhusu Kupanda cheo wajiendeleze kielimu.

Waziri Bashungwa amesema kuwa Mafundi sanifu ni jukwaa muhimu linalohitajika kwa maendeleo ya nchi hivyo waendelee kujituma na kujiamini kwenye matumizi ya teknolojia Ili kujitoa kwenye utegemezi wa teknolojia kutoka nje.

Sambamba na hayo amewataka mafundi sanifu  kubuni teknolojia zenye mahitaji ya ndani ya nchi kwani ukuaji wa teknolojia duniani na mataifa hubuni vitu ambavyo vina manufaa kwa nchi zao.

"Nawasihi bunifu za Teknolojia zisiishie kwenye karakana bali zitangazwe kwa ajili ya kukuza uchumi na kuongeza soko la ajira". Amesisitiza 

Awali msajili wa Bodi ya ERB, Mhandisi Bernard Kavishe , amesema madhumuni ya kukutanisha mafundi sanifu ni kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kada hiyo ikiwemo kukumbushana kuzingatia sheria na kanuni zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ERB Dk. Menye Manga amesema mafundi sanifu ni kada muhimu kwa maendeleo ya nchi hasa katika sekta za Ujenzi na viwanda.








Post a Comment

Previous Post Next Post