SERIKALI IMEDHAMIRIA KUENDELEA KUTEKELEZA AGENDA YA UCHUMI WA VIWANDA: DKT. BITEKO
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Serikali imedhamiria kuendelea kutekeleza kwa dhati agenda ya uchumi wa viwanda kwa kufanya uwekezaji wenye tija katika miundombinu wezeshi ya barabara, reli pamoja na umeme wa uhakika.
Sambamba na kuendelea kuimarisha nidhamu katika utendaji kazi, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara na uwekezaji pamoja na kutoa ahueni za kikodi kwa wawekezaji katika viwanda vya ndani na kuanza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara Tanzania.
Hayo yameelezwa Mei 24, 2024 jijini Dar es salaam na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akifunga Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Uganda.
“Sote ni mashahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuendelea kutekeleza agenda ya uchumi wa viwanda. Pamoja na kuweka msisitizo katika katika kukuza biashara na uwekezaji hususani viwanda vya kuongeza thamani kwa kutumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini kutokana na kilimo, kuongeza thamani ya madini yanayochimbwa nchini, kuongeza uzalishaji kupitia sekta ya viwanda na kuimarisha na kuboresha sekta ya fedha”, amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Serikali inaendelea kuhakisha kuna upatikanaji wa mafuta na gesi kwa bei nafuu na kuongeza ushiriki wa wananchi katika kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza kipato kwa wananchi wengi na kuleta uwiano mzuri wa kiuchumi na kijamii mijini na vijijini. Aidha, nguvu nyingi zinaelekezwa katika uwekezaji wa viwanda vya kimkakati kwa lengo la kuunganisha sekta mbalimbali na kuongeza uzalishaji na ukuaji mpana wa uchumi”.
Akizungumzia kuhusu kiwango cha biashara kinachofanywa kati ya Tanzania na Uganda, Dkt. Biteko amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Biashara la Kimataifa hadi kufikia mwaka 2023 urari wa biashara baina ya nchi hizi mbili ni kuwa, Tanzania iliuza nchini Uganda bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 310.67 na kwa upande wa sekta ya utalii jumla ya watalii 46,000 kutoka nchini Uganda walitembela vivutio mbalimbali nchini Tanzania katika kipindi hicho.
Aidha, kwa upande wa Uganda bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani dola millioni 154 ziliuzwa nchini Tanzania hadi kufikia mwaka 2023 na kuwa bado nchi zote mbili zina nafasi kubwa na muhimu ya kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na kukuza ushirikiano ulipo wa kibiashara na kidiplomasia ambao umedumu kwa muda mrefu.
Licha ya uwepo wa mradi wa bomba la mafuta kati Tanzania na Uganda, Dkt. Biteko amesema “Tunayo makubaliano kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yetu tunajenga bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Uganda ili wenzetu waweze kunufaika kwa kutumia gesi iliyopo Tanzania kukuza uchumi wao na tunajenga bomba la mafuta safi kutoka Tanzania hadi Uganda. Pia, tumeamua kwa pamoja kujenga njia ya pamoja ya umeme kutoka Ibadakuli mkoani Shinyanga hadi Mbarale nchini Uganda yenye urefu wa km 610 ambayo itazalisha kv 400 ili kusaidiana katika changamoto za umeme.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi anayeshughukia Masuala ya Kikanda wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. John Mulimba amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa jitihada zao za kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, ameongeza kuwa kupitia Kongamano hilo la Biashara kati ya Tanzania na Uganda, kwa upande wa nchi yake itahakikisha inafanyia kazi changamoto zilizojadiliwa kwa kutatua vikwazo vya biashara.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli amesema kuwa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda itaendelea kushirikiana na Jukwaa hilo sambamba na kuwakaribisha Watanzania na Waganda kufika ubalozini endapo watahitaji huduma katika kufanya shughuli za biasharana na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Kongamano hilo la pili la biashara kati ya Tanzania na Uganda lenye kaulimbiu “Enhancing Our Win - Win partnerships” ni mwendelezo wa kongamano la kwanza lililofanyika Septemba 2019 jijini Kampala nchini Uganda na kuhudhuriwa na washiriki 250 likiwa na kauli mbiu isemayo “Promoting Bilateral Trade and Investment for Growth and Sustainable Development” inayoendana na ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhusu kujenga uchumi endelevu kwa kupitia biashara na uwekezaji.
Aidha, Kongamano hilo la pili ni muhimu kwa Taasisi za Serikali na sekta binafsi katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya biashara na uwekezaji na kubadilishana mawazo juu ya fursa zilizopo baina ya nchi hizo mbili na namna ya kushirikiana ili kuleta ufanisi na kuinua mchango wake katika uchumi wa nchi hizo.
Mada zilizojadiliwa katika Kongamano hilo ni pamoja na mashirikiano ya uwili katika sekta za kipaumbele, kuimarisha fursa za kibiashara na uwekezaji baina Uganda na Tanzania, fursa na changamoto zilizopo katika mnyororo wa thamani wa madini na maendeleo endelevu na ushirikiano kwenye nishati, ambapo pia mikutano kadhaa imefanyika baina ya wafanyabiashara wenyewe kwa wenyewe na wafanyabiashara na Serikali pamoja na kuingia mikataba mbalimbali.