TAMASHA LA KILIMANJARO CULTURAL FESTIVAL KUKUZA UTALII MKOANI KILIMANJARO
Na,Happiness Shayo-Kilimanjaro
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival linalohusisha utamaduni wa vyakula ,ngoma na lugha za asili za jamii ya Wachaga, Wapare na Wamaasai litasaidia kukuza utalii wa Mkoani Kilimanjaro endapo litaendelezwa na kutumika ipasavyo.
Amesema lengo la Tamasha hilo ni kukuza na kuhamasisha utalii wa malikale ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro sambamba na kuenzi mila na desturi za jamii za Mkoa huo zinazojumuisha Wapare, Wachaga na Wamaasai.
Ameyasema hayo leo Desemba 28,2023 alipokuwa akifunga tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Kili Home Garden, Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro.
“Nimeshuhudia vyakula vya kiasili vya jamii za Mkoa wa Kilimanjaro vilivyoandaliwa kwa ustadi mkubwa, tukio hili limenikumbusha masuala ya afya kuhusu umuhimu wa vyakula vya asili ikiwa ni pamoja na kukinga miili yetu na kujenga nguvu mwilini na hii ndiyo sababu zamani Wazee wetu waliishi miaka mingi bila ya kusumbuliwa na maradhi ya mara kwa mara.” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Pia, amesema ameshuhudia ngoma za asili za kipare, kimaasai na kichaga, lugha za asili za Kipare, Kimaasai na Kichaga ambazo zinawakumbusha vijana kuenzi mila na tamaduni zao ili waweze kufahamu walikotoka na wanakoelekea.
“Natoa wito kwa vikundi vya ngoma kuendelea kukutana kila wakati na kubadilishana uzoefu baina ya kikundi kimoja na kingine kwa sababu ngoma za asili ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaokuja kutembelea vivutio vyetu nchini Tanzania” Mhe. Kairuki amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki amezindua program ya ‘’Kilimanjaro Home Stay’’ inayohusu utaratibu wa kutumia nyumba za wenyeji kutoa huduma za malazi kwa wageni hususan kipindi cha matukio makubwa kama vile mbio za Kilimanjaro Marathoni ili kukuza vipato kwa jamii moja kwa moja.
Ameipongeza Taasisi ya Kilimanjaro Cultural Festival kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kufanya utafiti na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za Urithi wa Utamaduni usioshikika wa jamii ya Kilimanjaro ikiwa ni pamoja na kuandaa kanzidata ya maeneo ya malikale yaliyopo ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Naye,Mwenyekiti wa Kilimanjaro Cultural Festival, Hans Mmasi amesema tamasha hilo linaunga mkono juhudi za Serikali za kutangaza utalii nchini na linalenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya utalii, utamaduni na biashara.
Ameongeza kuwa tamasha hilo lina matarajio ya kuvutia wageni na watalii wapatao elfu kumi ifikapo mwaka 2028.
Tamasha hilo limeratibiwa na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Kilimanjaro Cultural Festival ambayo ilitokana na Jukwaa au Group la Whatsapp lijulikanalo kama ‘’Kilimanjaro Maendeleo Group’’, ambalo kwa sasa lina wanachama wapatao 400.
Tamasha hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiongozi wa Machifu wa Jamii za Mkoa wa Kilimanjaro, Mangi Frank Mareale, Viongozi wa Dini, Viongozi Mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.