FANYENI KAZI ZENYE MATOKEO CHANYA - DKT. BITEKO
Na,Mwandishi wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewasisitiza Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya kazi kwa ushirikiano ili kazi hizo zilete matokeo chanya kwa wananchi.
Aliagiza hayo hivi karibuni wakati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko walipozungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo katika kikao kilicholenga kufahamiana, kujumuika pamoja, kujikumbusha majukumu ya kazi na kufanya Tathmini ya Utendaji Kazi ili kuongeza ufanisi.
Mhe. Majaliwa aliwataka watumishi hao kuwahudumia Watanzania kwa weledi ili kuisaidia Serikali, kuwa wabunifu katika utendaji kazi, kusimamia Sera ya Uhifadhi wa Mazingira na kuwajibika kuwahudumia Watanzania.
Aidha, Dkt. Biteko aliahidi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa Ofisi hiyo katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali na kuwataka Watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano.
"Ninawaomba watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mnifundishe, mnielekeze, na kuniombea ili tufanye kazi kwa pamoja kuwahudumia Watanzania na kazi hizo ziwe chachu ya kuboresha maisha ya Watanzania na kupunguza umaskini ," alisema Dkt. Biteko.
Kikao hicho kilifanyika mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali katika Ofisi ya Waziri Mkuu.