MAJALIWA ASISITIZA NIDHAMU, MAADILI, UBUNIFU KWA WATUMISHI WA UMMA


MAJALIWA ASISITIZA NIDHAMU, MAADILI, UBUNIFU KWA WATUMISHI WA UMMA

Na,Mwandishi wetu-Dodoma

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wafanye kazi kwa bidii, weledi, nidhamu, uadilifu na ubunifu ili kutimiza maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Amesema kila mtumishi anapaswa kutambua kuwa mafanikio katika utekelezaji wa majukumu, mipango na mikakati wanayoisimamia yanahitaji juhudi ya kila mtumishi na nidhamu katika kufanya kazi.

Ametoa wito huo leo Jumamosi Novemba 11, 2023 katika kikao na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini Dodoma.

 “Nitoe wito kwa kila mtumishi kuzingatia nidhamu ya kazi na maadili ya utumishi wa umma, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza falsafa ya Kazi Iendelee. Kwa msingi huo watumishi wote wa umma mnao wajibu wa kufuata na kutekeleza falsafa hii. ”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza watumishi hao kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao vizuri na kwa weledi. “Kujituma kwenu, ushirikiano na bidii vimewezesha Serikali na hususan Ofisi ya Waziri Mkuu kupata mafanikio makubwa. ”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa tangu Rais Dkt. Samia aingie madarakani amekuwa anatoa msukumo wa kuboresha mazingira ya watumishi na kusisitiza kushughulikia stahiki mbalimbali za watumishi wa umma ikiwemo ulipaji wa malimbikizo ya mishahara, upandishaji wa madaraja na utoaji wa ajira mpya.

 “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amelipa madai malimbikizo ya mishahara ya watumishi 121,858 yenye jumla ya shilingi bilioni 207.97, pia amepandisha madaraja watumishi 91,841 na shilingi bilioni 73.4 zimetumika kuwalipa watumishi hao”  

Pia, Mheshimiwa Majaliwa aliwakumbusha watumishi hao kusimamia kikamilifu na kwa makini miradi na programu zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili Ofisi isipoteze fursa ya kuungwa mkono na Taasisi za Kimataifa “Endeleeni kutoa huduma bora za Serikali kwa umma pamoja na kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali katika sekta zote kwa ufanisi na tija. ”

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewashukuru watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano wanaoendelea kumpa katika majukumu yake ya kila siku.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama amesema kuwa wataendelea kusimamia mipango ya kitaifa na ya kisekta kwa uaminifu mkubwa ili kuleta matokeo chanya Serikalini

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili waweze kufanikiwa kutekeleza ipasavyo majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufanisi wa hali ya juu.

Post a Comment

Previous Post Next Post