KUNDI LA VIJANA WA UMRI WA MIAKA 15 HADI 24 LINACHANGIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU KWA ASILIMIA 40- MHE. MHAGAMA



KUNDI LA VIJANA WA UMRI WA MIAKA 15 HADI 24 LINACHANGIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU KWA ASILIMIA 40- MHE. MHAGAMA

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Jamii imetakiwa kuwa mstari wa mbele  katika kuongoza kutokomeza maambukizi ya ukimwi nchini ambapo Takwimu zinaonesha kuwa kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo Novemba 14,2023  jijini Dodoma na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama kuhusu maadhimisho ya ukimwi Duniani ambayo yanatarajiwa kufanyika Kitaifa Mkoani Morogoro huku waziri Mkuu kasimu majaliwa akitarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

"Nguzo kubwa katika kutimiza ndoto yetu ya kumaliza VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030 na Maeneo yanayohitaji msukumo na
vipaumbele ni pamoja na kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa vijana kwani takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40 na hivyo kulifanya kundi hili kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya VVU". Amesema.

Aidha,Mhe. Mhagama ametaja Matukio yaliyopangwa kufanyika katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI ya mwaka 2023 Kitaifa ni pamoja na Maonesho ya Shughuli za Wadau wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini yatakayoanza tarehe 24 Novemba, 2023
hadi 1 Desemba 2023.

"Uzinduzi rasmi wa wiki ya Maadhimisho haya utafanyika Tarehe 24 Novemba, 2023 Mkoani Morogoro,Uzinduzi huu pia utaambatana na maandamano ya Wadau wa Udhibiti UKIMWI, Mdahalo wa Viongozi wa Dini na kijamii pamoja na vijana utakaofanyika tarehe 25 Novemba, 2023 kwenye Ukumbi wa Mikutano ulioko Hoteli ya Nashera, Morogoro". Amesema

"Kongamano la Kisayansi la Kitaifa la kutathmini Hali na mwelekeo wa udhibiti wa VVU na UKIMWI nchini litakalofanyika tarehe 27 hadi 28 Novemba, 2023 katika Ukumbi wa Nashera, Morogoro pamoja na Utoaji huduma rafiki kwa vijana litakalofanyika tarehe 30 Novemba 2023 ambapo Vijana watatengewa eneo maalumu litakalojulikana kama Kijiji cha Vijana ndani ya uwanja wa Jamhuri, Morogoro". Ameongeza 

Sambamba na hayo,Mhe. Mhagama  ameelekeza Mikoa yote nchini,Chini ya uratibu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuandaa na kuadhimisha siku hii ya Maadhimisho ya ukimwi Duniani.

"Kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini
kusimamia utekelezaji wa shughuli hii kwa kushirikiana na wadau wa kudhibiti VVU na UKIMWI walioko kwenye Mikoa yao". Amesisitiza.

Hata hivyo, Mhe. Mhagama anawahamasisha na kuwakaribisha wananchi hususani wa Mkoa wa Morogoro na Mikoa jirani kushiriki kwenye Kilele cha Siku ya UKIMWI.

"Kutokana na umuhimu wa maadhimisho haya, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku hii
katika ngazi zote nchini ikiwa ni pamoja na familia, sehemu za kazi, nyumba za ibada, shuleni, vyuoni na katika jumuiya mbalimbali kuadhimisha siku hii kwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma na kushiriki kwenye matukio yanayohusiana na maadhimisho haya kwenye maeneo yao". Amesema 

Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa kudhibiti Ukimwi kutoka  Wizara ya Afya Dkt. Anath Rwebemberwa amesema wizara imekuja na mkakati wa kusambaza Kondomu ili kudhibiti watu kuchukua Kondomu nyingi badala ya kuchukua Mbili au tatu kwa matumizi yake.

"Sasa hivi tunaenda kupanga usambazaji mwingine mpya wa usambazaji wa Kondomu mana mfumo ambao uliopo Sasa unakuta mtu anachukua Kondomu nyingi Kwa matumizi yake na hata kuziuza,hivyo utaratibu tutakaokuja nao utaruhusu mtu kuchukua kondomu tatu tu". Amesema

Naye Dkt. Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, amesema matokeo ya tiba yanaonesha kuwa wanaume ni wavivu kwenda kupata huduma ya Tiba.

"Wanaume ndiyo wanakufa zaidi kwa ugonjwa wa ukimwi kuliko wanawake kwa sababu hawapimi na hawaendi Kwenye huduma, hivyo wanaume jitikezeni kupima ili mjue hali zenu". Amesema

Maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani kwa mwaka huu 2023 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI” ambapo maadhimisho hayo yataadhimishwa ndani ya wiki moja ambapo shughuli mbalimbali zinazohusu Utoaji wa taarifa za udhibiti wa VVU na UKIMWI na huduma ya Upimaji wa Hiari wa VVU zitafanyika kuanzia tarahe 24 Novemba, 2023 hadi siku ya kilele ya tarehe 1.disemba 2023.


Post a Comment

Previous Post Next Post