MASOKO NA VITUO VYA UNUNUZI WA MADINI YACHANGIA SHILINGI BILIONI 157.4-MHANDISI LWAMO
Na,Mwandishi wetu-Dodoma
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa kutokana na usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022-2023 mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli, utoaji wa leseni za madini na masoko ya madini kuchangia kwenye makusanyo ya Serikali hali iliyochangia Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi.
Mhandisi Lwamo ameyasema hayo leo Agosti 18, 2023 kwenye mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dodoma ulioratibiwa na Idara ya Habari- MAELEZO kwa ajili ya kuelezea mafanikio ya Tume ya Madini katika kipindi cha mwaka mmoja (2022-2023) sambamba na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023-2024.
Akielezea mafanikio kwenye ukusanyaji wa maduhuli, Mhandisi Lwamo amesema kuwa, kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kilipanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa mwaka 2021/2022 na kufikia Shilingi bilioni 678.04 mwaka wa fedha 2022/2023, makusanyo haya ni sawa na asilimia 82.49 ya lengo la mwaka ambalo lilikuwa ni shilingi bilioni 822.
katika kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini,Mwaka wa Fedha 2022/2023, Tume ilifanikiwa kutoa jumla ya leseni za madini 9,642 kati ya leseni 9,174 zilizopangwa kutolewa zikiwemo leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, Biashara ya Madini pamoja na Uchenjuaji wa Madini.
Ameongeza kuwa kati ya leseni zilizotolewa, leseni 6,511 sawa na asilimia 70.97 zilitolewa kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya sita katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuongeza mchango wao katika Sekta ya Madini.
Hali ya masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, Mhandisi Lwamo amesema kuwa Tume ya Madini kupitia Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini ilifanikiwa kuanzisha jumla ya Masoko ya Madini 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa Madini 94 nchini mapema Machi 17, 2019 kama mkakati wa kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini nchini ili kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini kwa Serikali.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 masoko na vituo vya ununuzi wa madini vilichangia jumla ya shilingi bilioni 157.4 kama mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini ikiwa ni sawa na asilimia 23.22 ya makusanyo yote yaliyokusanywa na Tume katika mwaka husika.
Katika hatua nyingine akielezea mchango na ukuaji wa Sekta ya Madini, Mhandisi Lwamo amesema kuwa, katika mwaka wa 2022 mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa ulikuwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na Mwaka 2021 ambapo ulikuwa asilimia 7.2.
“Vilevile ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.6 Mwaka 2021 hadi 10.9 Mwaka 2022. Tunaamini tutaweza kufikia mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa wa asilimia 10 au zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 na Dira ya Maendeleo ya Taifa. amesema Mhandisi Lwamo.
Hata hivyo, ameeleza mafanikio ya Tume kwenye usimamizi wa usalama wa afya na mazingira kwenye migodi ya madini nchini,.ambapo amesema Tume ilifanikiwa kufanya ukaguzi kwenye migodi midogo 19,580 iliyopo katika mikoa ya kimadini ya Morogoro, Tabora, Arusha, Kahama, Mwanza, Tanga, Manyara, Iringa, Njombe, Mbogwe, Shinyanga, Dodoma, Kigoma, Kagera, Chunya, Geita, Mara, Mbeya, Rukwa, Lindi, Ruvuma, Mtwara, Songwe, Pwani, Dar es Salaam na Katavi sambamba na kutoa elimu kuhusu usalama, afya, matumizi salama ya baruti na utunzaji wa mazingira migodini.
Aidha, Mhandisi Lwamo amesisitiza kuwa katika kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali madini, Tume imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa wamiliki na waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.
“ Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022-2023 jumla ya mipango 656 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi ambapo kati ya mipango iliyowasilishwa, 652 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa,” amesema Mhandisi Lwamo.
Mhandisi Lwamo amewataka watanzania na wadau wa madini kutoka nje ya nchi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Madini sambamba na kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake.