MASHINE YA MRI IMEANZA KUFANYA KAZI HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA -MBEYA
Na,Mwandishi wetu-Mbeya.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo tarehe Julai 12, 2023 imeanza rasmi kutoa huduma ya vipimo kwa kutumia mashine ya kisasa ya uchunguzi wa magonjwa MRI (Magnetic Resonace Imaging).
Akiongea baada ya kumaliza ziara yake hospitalini hapo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa mashine hiyo ambapo ambayo imekua ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya na kutoa upatikanaji bora wa vipimo vya kisasa kwa wananchi.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kufanya uwekezaji huu katika katika Mkoa wa Mbeya ambapo kufanya kazi kwa mashine ya MRI italeta mabadiliko makubwa katika huduma za afya na kuimarisha uwezo wa Hospitali yetu na wataalamu wetu kutoa huduma bora kwa jamii na kupunguza gharama za kusafiri kwenda Dar es salaam kuifuata huduma hii” ameshukuru Mhe. Homera
Aidha Mhe. Homera ameishukuru Wizara ya Afya chini ya Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa jitihada kubwa zilizofanyika hadi kufanikisha shughuli za usimikaji wa mashine hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia takribani wakazi wa mikoa 7 ya Nyanda za Juu Kusini.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji amesema uwepo wa mashine hiyo utawezesha shuguli za huduma hospitalini hapo kufanyika kwa ubora zaidi kwa kuwa hapo awali wataalamu walikuwa wakilazimika kutoa rufaa kwa wagonjwa kwenda Dar es salaam kufuata kipimo cha MRI.
“Tunaweza kupima wagonjwa ambao wana matatizo ya Saratani au vimbe za aina tofauti tofauti kwenye mwili, pia tunaweza kupima mabadiliko yanayoendana na umri.”
Akizungumza mara baada ya kupata huduma za uchunguzi kupitia mashine ya MRI, Bi. Reinfrida Kayombo mkazi wa Jijini Mbeya, ameishukuru Serikali kwa kwa kuwaletea huduma hiyo karibu na kuwasaidia kwa wakazi wa Nyanda za juu kusini ambao hapo awali walilazimika kutumia garama kubwa kuifuata huduma hiyo mbali.
“Tunamshukuru sana Mama Samia kwa kutuletea huduma hii maana hapo awali tulikuwa tunapata gharama kubwa kusafiri lakini kwa sasa tumeletewa huduma hapahapa.” Amesema Bi. Kayombo.
Mashine ya MRI ni teknolojia ya hali ya juu ambayo inatumika kuchunguza na kutoa picha za mwili wa binadamu kwa kutumia mawimbi ya umeme na magneto. Mashine hiyo inatoa maelezo ya kina na inaweza kuchunguza hali mbalimbali za kiafya, kama vile matatizo ya ubongo, saratani, magonjwa ya moyo, na matatizo ya mfumo wa musculoskeletali. Uwepo wa mashine hiyo utasaidia wakazi Mikoa saba ya Nyanda za Kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Njombe na Iringa pamoja na nchi za jirani kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na tiba kwa haraka Jirani na maeneo waliyopo.