CHEMBA YA MKOSHA RC SENYAMULE KWA KUPATA HATI SAFI

 


CHEMBA YA MKOSHA RC SENYAMULE KWA KUPATA HATI SAFI

Na Mwandishi wetu,Chembe Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kwa kupata hati safi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichojadili taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 .

Pongezi hizo amezitoa leo Julai 14, 2023 wakati wa kikao kazi cha Baraza la Madiwani katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo Mkoani Dodoma.

"Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilikuwa na hoja 50 ambazo ambazo zimegawanyika katika sehemu tatu, hoja za mwaka jana 25, hoja za miaka iliyopita 25 na agizo la LAAC ambalo ni moja" ameeleza Mhe.Senyamule

Aidha, amesema kati ya hoja 50, 13 zimefungwa na 37 bado zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji chini ya Menejimenti ya Halmashauri chini ya usimamizi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Mhe. Senyamule amewaasa kufanya kazi kwa bidii,kuondoa tofauti baina yao na kutafuta namna nzuri ya usuluhishaji wa tofauti zao zilizopo ili kuleta tija katika kuwatumikia wananchi.

‘’Chemba ni miongoni mwa Halmashauri ambazo taarifa za septemba 2022 zinaonyesha kuwa na tofauti katika taarifa zenu hivyo jitahidini kutafuta namna inayofaa kupata usuluhishi ili ziweze kuendana ili kupunguza hoja za ukaguzi kila mwaka” Senyamule amesisitiza

Mhe.Senyamule amesisitiza kamati za fedha zinazokutana kila mwezi ziwe na agenda ya kudumu ya kujadili mwenendo wa ujibuji wa hoja za ukaguzi za Mkaguzi wa ndani ili Halimashauri kuondokana na changamoto ya kuwa na hoja nyingi zisizofanyiwa kazi .

Vile vile ameagiza Halmashauri hiyo kuweka mikakati ya kuhakikisha mapato yanaongezeka kufikia bilioni 2 kwa kufanya ubunifu mbalimbali wa vyanzo vya mapato.

Aidha amewataka kuhakikisha wanakamilisha Miradi ya maendeleo kwa wakati na ubora unaotakiwa ili kuendana na kasi ya viongozi wanayotoa hela ikiwa ni pamoja na miradi ya fedha za SEQUIP .

Kwa Upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Ally Gugu amewaasa Watumishi kuendeleza kushirikiana na Utawala vizuri ili kurahisisha utendaji na kufuata Sheria, taratibu, kanuni za utumishi wa umma bila kupoteza muda katika utendaji kazi .

Post a Comment

Previous Post Next Post