Na Mwandishi wetu
Katika Kuelekea sherehe za miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amezindua mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhi majisafi lenye ujazo wa lita milioni 2.5 katika eneo la Buigiri, Wilayani Chamwino Jijini Dodoma.
Aidha mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 1.6 badala ya 2.5 utawezesha kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 42 mpaka 87 katika wilaya ya Chamwino.
Akizungumza leo Aprili 25, Wilayani Chamwino wakati wa uzinduzi wa Mradi huo Mhe.Senyamule,amesema kuwa maandalizi ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa mkoa wa Dodoma unaendelea kwa kuzindua miradi mbalimbali ya kimaendeleo ukiwemo huo wa maji.
Pia,Mh.Senyamule amewahakikishia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Chamwino kuja kuwekeza kwani kuna uhakika wa upatikanaji wa maji hivyo ni eneo salama kwa uwekezaji.
''Kila mwekezaji ambaye alikuwa anataka kuja kuwekeza Chamwino kitu cha kwanza alikuwa akiulizia Maji akiambiwa hakuna anakata tamaa kwa sasa maji yamekuja wenye nia ya kuwekeza Chamwino Njooni Neema ya Maji imekuja Chamwino''amesema Senyamule.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema kwa takwimu za Kitaifa upatikanaji wa maji kwa vijijini ni 37% huku upande wa mjini 88% wanapata maji.
Kemikimba ameongeza kuwa miradi inayotekelezwa kwa Mkoa wa Dodoma ni uchimbaji wa Visima maeneo ya pembezoni ambapo Bilioni 4.8 zitatumika eneo la Nzuguni kuchimba visima ambapo utazalisha maji lita milioni 7 kwa siku na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka 2023.
Hata hivyo baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Chamwino wametoa shukrani Kwa Rais Samia pamoja na Mamlaka ya Maji Mkoani Dodoma kwa kuzindua kisima hicho kutokana na adha walizokuwa wanakumbana nazo huku wakisema mradi huo umeleta neema wilayani hapo.
