BUWSSA YAWEKA MIKAKATI YA KUPUNGUZA UPOTEVU WA MAJI PAMOJA NA KUANZA KUJENGA MIUNDOMBINU YA MAJI TAKA.
Na,Saleh Lujuo-Dodoma.
Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Bunda imeweka mikakati ya kupunguza upotevu wa maji ikiwa ni mpango mkakati wa kupunguza upotevu wa maji wa miaka mitatu ulioanza mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2023/2024 unaoendana na mpango wa kibiashara wa Mamlaka ya maji.
Akitoa Taarifa ya utendaji Kazi na Muelekeo wa kufikia Asilimia 95 ya huduma ya maji Mjini Bunda Kwa mwaka 2025, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bunda Esther Gilyoma amesema Mamlaka hiyo imeandaa andiko la mradi kwa ajili ya kukopa fedha kiasi cha TShs 815,000,0000 katika mfuko wa maji ili kuhakikisha upotevu wa maji unapungua kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024.
“Mkakati huu ambao tunao najua itaenda kutokomeza kabisa upotevu wa maji katika Wilaya ya Bunda, hivyo wananchi waendelee kutunza miradi yetu ya maji”.amesema Gilyoma.
Akizungumzia hali ya huduma ya maji na usafi wa mazingira,Mkurugenzi huyo ametaja kutokuwepo na huduma ya maji taka katika Mji huo ambapo amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wanategemea kuanza kujenga miundo mbinu ya majitaka eneo la Butakale liliyoko Mjini Bunda.
"Kwa sasa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bunda haina huduma ya majitaka,hivyo magari ya watu binafsi ambayo yanasimamiwa na Halmashauri ya mji wa Bunda ndiyo yanatumika katika kutoa huduma za majitaka.Hivyo kupitia Mamlaka ya maji Bunda kwa mwaka wa fedha 2023/2024 tunategemea kuanza kujenga miundo mbinu ya majitaka eneo la Butakale liliyoko Mjini Bunda". amesema Gilyoma.
katika kufanikisha mpango endelevu wa kufikia asilimia 95% ifikapo 2025 Mamlaka hiyo imedhamiria Upanuaji wa mtandao wa bomba hasa kwa maeneo ambayo mtandao wa maji haujafika eneo la Sazira, Mcharo, Wariku, Guta, Kunzugu na Manyamanyama.
Sambamba na hayo Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bunda imeomba kuongezewa eneo la utendaji la Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Busega,Kibara na Nyamswa Kwa lengo la kuboresha huduma, kuongeza idadi ya wateja ambao watasaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kupunguza gharama ya bili ya maji.


