TANZANIA NCHI YA TANO DUNIANI KWA KUWA NA WAGONJWA WENGI WA SIKOSELI.

TANZANIA NCHI YA TANO DUNIANI KWA KUWA NA WAGONJWA WENGI WA SIKOSELI

Na,Saleh Lujuo-Dodoma.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, zaidi ya watoto 300,000 duniani huzaliwa na Sikoseli kila mwaka ambapo nchini Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto elfu kumi na moja (11,000) huzaliwa na ugonjwa wa sikoseli kila mwaka ambayo ni sawa na watoto 11 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa. 

Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya tano duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Sikoseli ambapo kwa sasa Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 200,000 wenye Sikoseli. 

Takwimu hizo zimetolewa Leo Juni 19,2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika siku ya  sikoseli Duniani ambapo amesema takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto 7 kati ya watoto 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki nchini kutokana na madhara yanayohusiana na ugonjwa wa sikoseli.

"Nchi nyingine zenye wagonjwa wengi wa Sikoseli ni Nigeria, India, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Angola". ameongeza

"Inakadiriwa kwamba, hadi sasa Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 200,000 wenye Sikoseli.Vilevile, takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watoto 7 kati ya watoto 100 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki nchini kutokana na madhara yanayohusiana na ugonjwa wa sikoseli". amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema Katika kuboresha zaidi huduma kwa wagonjwa wa Sikoseli, serikali inaendelea kufanya tafiti za sikoseli nchini ambazo zitasaidia kupata takwimu na kufanya maamuzi ya Kisera yenye uthibitisho wa kisayansi unaoendana na mahitaji ya nchi  ili kuwa na kizazi kisichokuwa na ugonjwa wa sikoseli.

"Katika kuboresha zaidi huduma kwa wagonjwa wa Sikoseli, Serikali imeanzisha kliniki katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa pamoja na Hospitali za wilaya hapa nchini ambapo Ongezeko la mahudhurio ya wagonjwa wa Sikoseli kutoka 49,025 mwaka 2018 hadi kufikia 86,990 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 56". amesema Waziri Ummy.

Akitoa taarifa ya hali ya ugonjwa wa sikoseli kwa Mkoa wa Dodoma, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dr. Nelson Bukuru, amesema idadi ya Wagonjwa wa seli mundu wanazidi kuongezeka hasa wale wanaokuja kuonwa kwenye kliniki walifikia wagonjwa 559 mwaka 2023 kutoka wagonjwa 380 mwaka jana (2022).

"tunaomba Serikali kuwezesha upatikanaji wa mashine za kufanya uchunguzi wa sikoseli kwa watoto wachanga wanaozaliwa kwenye vituo vya huduma za Afya ili watakaogundulika na tatizo waweze kupata matibabu kwa wakati" amesema Dr.Bukuru.

Kwa upande wake Mkurugenzi idara ya Tiba wa wizara ya Afya Prof Paschal Ruggajo amesema wanaendelea kutoa elimu ya kupunguza uwezekano wa kupata watoto waliorithi vinasaba vya sikoseli kwa kuhamasisha ushauri na upimaji wa vinasaba vya siko seli kwa vijana kabla ya kuingia kwenye mahusiano.

Kila ifikapo tarehe 19 Juni, ya kila mwaka,Tanzania huungana na mataifa mengine Duniani katika kuadhimisha Siku ya “Sickle cell” Duniani ambapo 
Ugonjwa wa sikoseli husababishwa na kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi wote wawili. Takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 15-20 ya watanzania 100 wana vinasaba vya ugonjwa huu, yaani wana uwezekano wa kupata watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli iwapo watakuwa na wenza wenye vinasaba vya Sikoseli.

Post a Comment

Previous Post Next Post