EWURA YAZINDUA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA PAMOJA WA MIUNDOMBINU ILIYOKO CHINI YA ARDHI KWENYE MIKUZA INAYOTUMIWA NA TAASISI NA KAMPUNI ZA HUDUMA MBALIMBALI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma.
Mamlaka ya udhibiti wa Matumizi ya Nishati na Maji (EWURA) imezindua Mwongozo wa Usimamizi wa Pamoja wa Miundombinu iliyoko Chini ya Ardhi Kwenye Mikuza (wayleave) wa Mwaka 2023 kwa dhumuni la kuimarisha usalama wa umma, kuongeza uadilifu na usimamizi makini wa miundombinu iliyopo chini ya ardhi.
Hatua hiyo ni Katika kudhibiti changamoto za miundombinu mibovu iliyoko chini ya Ardhi Kwenye MIKUZA inayotumiwa na na Taasisi na Kampuni za huduma mbalimbali hapa nchini.
Akizindua Mwongozo huo leo jijini Dodoma,Kamishna Wa petrol na Gesi wa wizara ya Nishati, Michael Mjinja amewataka wamiliki na watumiaji wa mikuza kufuata Mwongozo huo ili kuleta ufanisi katika kazi zao kwa dhumuni la kuimarisha usalama wa umma, kuongeza uadilifu na usimamizi makini wa miundombinu iliyopo chini ya ardhi.
"Mwongozo huu nitakaouzindua leo utasaidia katika kuratibu shughuli za ujenzi, uendeshaji, marekebisho na matumizi mengineyo ya mikuza inayotumiwa kwa pamoja na wadau mbalimbali bila kuathiri usalama wa miundombinu, umma na mali zao,Hivyo basi, niwatake wamiliki na watumiaji wa mikuza kufuata mwongozo huu pindi wanapofanya shughuli zao" amesisitiza Mjinja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt,James Andilile Amesema baada ya maandalizi ya muda mrefu, timu ya wataalamu imekamilisha maandalizi ya mwongozo huo na rasimu ya mwongozo ilipitiwa na wamiliki na watumiaji wa mikuza.
"Mwongozo huu utaratibu shughuli za ujenzi, uendeshaji, marekebisho na matumizi mengineyo ya mikuza na leo tuko hapa kwa uzinduzi rasm na kwa usalama wa miundombinu iliyoko chini ya ardhi tunaamini wamiliki na watumiaji, wataufuata mwongozo huu katika utumiaji wa mikuza ili kulinda miundombinu hiyo, kuepusha migogoro na kuokoa maisha ya watu na mali zao" Amesema Dkt Andilile.
Naye Mwenyekiti Wa JSC Mhandisi Michael Mgondo amesema Kamati ya Kiufundi ya Pamoja (Joint Technical Committee - JTC) ilipewa jukumu la kuandaa Mwongozo wa usimamizi wa pamoja wa miundombinu iliyoko chini ya ardhi kwenye mikuza (wayleave) ambapo Mwongozo huo uliandaliwa kwa kuainisha vipengele vyote muhimu vya kitaalam na kiusalama.
"Makubaliano haya yalihusisha Taasisi na kampuni zifuatazo TAZARA, TAZAMA, SONGAS, TPDC, GASCO, TRC, TTCL, M&P LIMITED, TANROADS, PAET, TANESCO, DAWASA na TARURA na juhudi hizi hazijafikia Taasisi na Kampuni zote zenye miundombinu chini ya ardhi kwa mfano mamlaka za maji mikoani, kampuni za mawasiliano na kampuni za madini" Amesema Mgondo.