VIONGOZI WA AFRIKA WATAKIWA KUWEKEZA KWA WATU NA KUTOA KIPAUMBELE KWA VIJANA NA WANAWAKE.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Summit) utakaofanyika nchini tarehe 25 - 26 Julai, 2023. 


Mhe. Dkt. Samia ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kuendelea kuchukua hatua kwa kuwekeza kwa watu na kutoa kipaumbele kwa vijana na wanawake.


Mhe. Rais pia amewataka viongozi wa Afrika kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wengi kwa kuwekeza zaidi katika kuboresha afya za watu, maji safi na salama, elimu bora na ujuzi muhimu kwa maendeleo ya rasilimali watu.


Viongozi wa Afrika lazima tuendelee kuchukua hatua kwa kuwekeza kwa watu na kutoa kipaumbele kwa vijana na wanawake. Nitoe wito kwa viongozi wa Afrika kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na changamoto zinazokabili rasilimali watu kwa kuwekeza zaidi katika kuboresha afya za watu, kuwaletea maji safi na salama, kutoa elimu bora na ujuzi muhimu kwa maendeleo ya rasilimali watu,” alisema Mhe. Samia 


Rais Samia amesema taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa nchi nyingi za Afrika ukitoa za Afrika Kaskazini zinakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wa malengo ya milenia ya uendelezaji rasilimali watu hali ikiwa chini ya wastani hasa katika maeneo ya elimu, afya na ulinzi wa jamii. 


“Hali ya afya ya uzazi, uwepo wa maji safi na salama na usimamizi wa maji taka bado ni changamoto kwa nchi nyingi huku ujumuishi wa kijinsia ukiwa na kasi ndogo na utekelezaji wa sheria za kulinda wanawake na watoto wa kike dhidi ya ubaguzi,unyanyasaji wa kijinsia, ndoa za utotoni na ukeketaji ukiwa mdogo na kuongeza kuwa kuwa hali ya ukamilishaji wa malengo ya milenia namba , 4, 5, 6 na 8 kwa nchi za Afrika hairidhishi na inaonesha hatari ya kutokamilika kwa malengo hayo kufikia mwaka 2030,” alisema Dkt. Samia.


Akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alisema kuwa kufanyika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Rasilimali Watu mwezi Julai 2023, kunatokana na jitihada za Serikali kuboresha ushirikiano na kuzingatia umuhimu wa rasilimali watu katika kukuza uchumi.


Post a Comment

Previous Post Next Post