RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSAN ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MIKATABA YA KUPELEKA HUDUMA YA MAWASILIANO VIJIJINI.

Na,Saleh Lujuo-Dodoma.R

ais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassani amewataka vijana kote nchini  kutumia mitandao vyema kwa maendeleo yao ili kulinda mila na silka zao pamoja na kutumia kujielimisha zaidi kuliko matumizi mengine yasiyo na manufaa.

Rais Dkt Samia Suluhu Hassani ameyasema hayo leo Mei 13,2023 Jijini Dodoma katika Hafla ya Utiaji saini wa Mikataba ya Miradi Miwili ya Ujenzi wa Minara ya Simu 758 Pamoja na Mradi Wa kuongea uwezo wa Minara 304 katika Maeneo ya vijijini ambapo ametoa maagizo kwa Makampuni ya Simu kuhakikisha kuwa minara yote inakamilika kwa mujibu wa mikataba, kwa ubora, vigezo na wakati. 

"Kwa upande wa Serikali tunakwenda kupunguza urasimu ili vibali vitoke mapema. Halmashauri na Taasisi zote zinazohusika na utoaji wa vibali ndani ya mwezi mmoja vibali vyote viwe vimetoka" Amesisitiza Rais.

Aidha, Dkt Samia ameagiza Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) ushirikiane na TARURA kuhakikisha njia zinapatikana katika maeneo ya vijijini inapokwenda kujengwa minara hiyo Pamoja na   REA kuwa na changamoto ya fedha ya kupeleka umeme kwenye vitongoji  wahakikishe nao wanafikisha umeme sehemu zote ambazo minara hii itajengwa ili  kusaidia kushusha gharama za mabando yanayotumowa.

"Naelekeza UCSAF kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kupanga mipango ya pamoja ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza na Waziri Nape Nnauye, nakuagiza kuangalia vyema Mfuko huu ili nao wakatimize majukumu yao tuliyowaelekeza wakafanye" Amesema Dkt Samia.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa wito kwa Makampuni ya Mawasiliano Tanzania kuendelea kuweka mitaji zaidi kwa kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wakati wote kuhakikisha kwamba suala la mawasiliano linaimarika.

"Mradi wa ujenzi wa minara 758 nchini, utajibu ushauri na maswali ya Wabunge kuhusu nini mpango wa Serikali wa kumuwezesha Mtanzania kushika chombo cha mawasiliano na kuzungumza kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, sasa mawasiliano yatasambaa nchi nzima" Amesema waziri Mkuu Majaliwa.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe.Nape Nnauye amesema Kupitia UCSAF, Serikali imefanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano kwa Watanzania takriban milioni 15 wanaoishi vijijini kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na UCSAF kwa pamoja na Makampuni ya Simu.

"Serikali kupitia UCSAF imeingia makubaliano na watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano vijijini katika kata 1,258 zenye jumla ya vijiji  3,704 na wakazi 15,194,118 ambapo jumla ya minara ya mawasiliano 1,380 itajengwa" Amesema Mhe.Nape

"Katika mikataba 19 ambayo Mfuko wa UCSAF umeingia na Watoa Huduma za Mawasiliano, Serikali imeweza kutoa ruzuku ya Shilingi bilioni 199.9, fedha hizi ni ushahidi wa Serikali inavyothamini na kuhakikisha kila Mtanzania hasa wa vijijini wanapata mawasilano" Amesema Mhe.Nape.

Akitoa Taarifa kuhusu utiaji saini Mikataba ya kupeleka huduma ya Mawasiliano vijijini, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema Mfuko huo ulitangaza zabuni ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo 763 na baada ya mchakato huo walipata maeneo katika Kata 713 ambayo minara ya mawasiliano 758 itajengwa. 

"Ushiriki wa Watoa Huduma katika zabuni hii wameweza kushiriki kwa asilimia 93, hii pia ni historia iliyowekwa katika ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi" amesema Justina.

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) litajenga minara katika Kata 104, Kampuni ya Vodacom Tanzania itajenga minara 190 katika maeneo mbalimbali, Kampuni ya Airtel Tanzania itajenga minara katika Kata 168, Kampuni ya Tigo Tanzania itajenga minara 262, Kampuni ya Viettel Tanzania itajenga minara 34 katika maeneo mbalimbali.

Post a Comment

Previous Post Next Post