JESHI LA POLISI LAWAONYA WAHALIFU AMBAO HAWATAKI KUACHANA NA VITENDO VYA KIHALIFU NA KUFANYA KAZI ZA HALALI.


Na,Saleh Lujuo-Dodoma.

Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kwa wahalifu ambao hawataki kuachana na vitendo vya kihalifu na kufanya kazi halali kuwa watambue wakifanya hivyo watakamatwa kwa njia yoyote ile na itakuwa aibu kwao na kwa familia zao.

Onyo hilo limetolewa na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, makao makuu ya Polisi Dodoma SACP. David Misime leo Mei 15,2023 mbele ya waandishi wa habari ambapo amesema Jeshi la Polisi linaendelea kupata mafanikio katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kutokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi.


“Mtakumbuka kuwa Mei 3,2023 yaliripotiwa mauaji ya Dkt. Isack Daniel Athumani ambaye alikuwa mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kerende kilichopo Tarime Rorya akitokea kazini, tukio hilo lilifanywa na watu ambao hawakuweza kufahamika kwa mara moja,”amesema.


Amesema uchunguzi unakamilishwa ili wahalifu waweze kufikishwa mahakamani.


“Pia, mtakumbuka Aprili 26,2023 katika mtaa wa Matulole, Kata ya Buhalahala mkoani Geita, kulitokea mauaji ya mfanyakazi mmoja wa GGM kwa jina la Milembe Selemani maarufu kama Hungwa yaliyofanywa na watu ambao hawakuweza kufahamika kwa wakati huo,”amesema.


Aidha, ameongeza kuwa kutokana na uchunguzi makini wa askari wanaochunguza matukio ya mauaji, wamefanikiwa kukamata watuhumiwa watatu na kuonyesha vielelezo walivyotumia pamoja na baadhi ya mali za marehemu ambapo wakati wowote watafikishwa mahakamani.


“Mtuhumiwa wa nne baada ya kupata taarifa ya kukamatwa kwa wahalifu wenzake na kwamba askari wamefika nyumbani kwake aliamua kujihukumu mwenyewe kwa kujinyonga,”ameongeza.


Amesema mtuhumiwa huyo aliyejinyonga alijulikana kwa jina la Pasory Lugodishu (Buchuchu) alijinyonga Mei 6,2023 kwa kutumia mkanda wa suruali katika pori la hifadhi ya Buhindi wilayani Sengerema.

Post a Comment

Previous Post Next Post