UTAFITI uliofanywa na serikali mwaka 2017/2018,katika mikoa sita ya Tanzania Bara ili kubaini idadi na sababu za watoto kuishi na kufanya kazi mitaani ulibaini jumla ya watoto 6,393 wanaishi na kufanya kazi mitaani ambapo idadi hiyo wavulana ni 4,865 na wasichana ni 1,528.
Takwimu hizo zilitolewa jana Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis,wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Tamima Haji Abass.
Katika swali lake mbunge huyo ametaka kujua kama kuna utafiti uliofanywa na serikali kujua sababu za uwepo wa watoto wa mitaani.
Akijibu swali hilo Mwanaidi ametaja mikoa sita iliyofanyiwa utafiti kuwa ni Dar es salaam,Dodoma,Mbeya, Mwanza,Arusha na Iringa.
Katika swali la nyongeza mbunge huyo ametaka kujua serikali ina mpango gani baada ya kutambua sababu ya uwepo wa watoto hao.
Mwanaidi akijibu swali hilo amesema serikali itaendelea na mikakati endelevu ya kutoa malezi bora kwa wazazi na matunzo ili kuwatunza watoto katika ngazi ya familia na itakutanisha watoto na wazazi wao.
Sambamba na Hayo naibu waziri huyo ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanakaa na watoto wao ili kupata malezi bora na kuwakumbusha kuwa mtoto wa mwenzio ni wako na wanastahiki kupata haki stahili kwa kuwa mtoto wa leo ni Taifa la kesho.
