VIONGOZI WA DINI TUTANGULIZE MAOMBI ILI TAIFA LIBAKI SALAMA-RC SENYAMULE
💧Serikali ya Mkoa wa Dodoma imewasisitiza wananchi na viongozi wa dini kwa Kila mmoja kutanguliza maombi pamoja na kuwasihi vijana kuachana na mikumbo ya kutaka kufanya machafuko disemba 9,2025 kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha amanai ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule wakati akifungua kikao maalumu cha maombi kilichowakutanisha viongozi wa dini ambapo amesema Serikali imeweka siku tatu kuanzia Disemba 7, 8 na 9 kuwa siku za maombi ya kuliombea Taifa utulivu na mshikamano.
“Kila mmoja ana wajibu wa kulinda amani. Wakati huu si wa kusubiri tu tarehe 9 itakuwaje; hatupaswi kulala leo ili kuhakikisha kesho kunakuwa na salama,” alisema Senyamule akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuchukua hatua.
Amesema viongozi wa dini wana nafasi ya kipekee katika kuhamasisha umoja, maelewano na kutuliza mioyo ya wananchi, hasa kipindi hiki ambacho kumekuwa na taharuki katika maeneo mbalimbali.
“Huu si wakati wa kulala usingizi. Huu ni wakati wa kushikana na kuzungumza lugha ya amani. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumetimiza wajibu wetu,” amesema.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuendelea kumuomba Mungu ili Tanzania ibaki kuwa nchi ya utulivu, upendo na mshikamano.
Kikao hicho cha maombi kilihudhuriwa na viongozi kutoka madhehebu mbalimbali, ambao walitumia nafasi hiyo kuiombea nchi na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazoweza kuchochea uvunjifu wa amani.
Wakati wa kufunga maombi hayo, Senyamule amesisitiza kuwa kuna watu wachache wanaotamani uvunjifu wa amani, hivyo wananchi wanaopenda amani wanapaswa kuendelea kupaza sauti na kuonesha umoja katika kipindi hiki cha siku tatu za maombi.
“Tusilale. Tuendelee kupaza sauti, tufanye wajibu wetu wa kidini, na kubwa zaidi tuungane kuhakikisha amani inaendelea kutawala,” amesesema.
Kwa upande wao, Viongozi wa Dini wamempongeza Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano mzuri na wametoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda amani, kuhimiza maadili, na kuijenga jamii inayofuata misingi ya utu na uadilifu.
Kadhalika,Viongozi hao wamewaomba Watanzania kujilinda na maneno ya lawama badala yake wajinyenyekeze na kujielekeza kuomba huruma ya Mungu ili amani itawale Nchini.
