KATAENI FUJO NA MAANDAMANO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29,2025-TEC


KATAENI FUJO NA MAANDAMANO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29,2025-TEC

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania TEC limetoa wito kwa waumini wa Kanisa hilo, Viongozi, wananchi na wadau wa siasa ambao hawaridhiki na mwenendo wa mchakato wa uchaguzi Mkuu nchini Kutafuta njia rafiki za kushughulikia changamoto zilizopo badala ya kutumia kauli chonganishi na kuhamasisha vurugu zinazoweza kuvuruga amani na taswira ya Taifa.

Tamko la Baraza hilo la Maaskofu lililoandaliwa na Maaskofu wote 35 wa Kanisa hilo nchini na kusainiwa na Rais wake Mhashamu Baba Askofu Wolfgang Pisa ba Katibu Mkuu Dkt. Charles Kitima likitolewa Oktoba 11,Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa 2025 limewasihi pia waumini wake na wananchi kwa ujumla kutoshiriki, kuratibu au kuhamasisha mipango ya Uvunjifu wa amani ili kulinda ustawi na maendeleo ya nchi.

"Tunawasihi Watanzania wote bila kujali imani zao, Chama au msimamo wao wa kisiasa kutojihusisha na dhamira yoyote itakayoandaliwa kwa kusudi la kuchochea maandamano, ghasia za machafuko, vurugu, uharibifu wa mali za umma na za binafsi" imesema Taarifa ya Kanisa hilo kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kanisa hilo pia limehimiza Viongozi, wananchi na mamlaka zote nchini kuendelea kuheshimu haki na maoni ya wengine hususan wale wenye maoni tofauti ya kisiasa ili kudumisha mshikamano wa Kitaifa kabla na baada ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania, likitaja Watawa, Viongozi wa Jumuiya, Vigango na parokia za kanisa hilo kutekeleza wito wa kuihubiri amani ili kuzuia haiba za watu wote wanaotaka kuvuruga amani na kuhamasisha fujo kupitia mitandao ya kijamii na maeneo ya kazi.

Baraza la Maaskofu pia kando ya kueleza kuwa halijihusishi na masuala ya siasa likiwajibika kutoa maoni na mtazamo wake kwa waumini, wananchi na serikali juu ya mambo muhimu kwa maendeleo na mustakabali mwema wa Taifa,  limetoa wito kwa Kiongozi atakayeshinda katika uchaguzi Mkuu kuwa tayari kuliunganisha Taifa na kuchukua hatua madhubuti za kuendeleza amani na mshikamano kwa maendeleo ya Tanzania

Post a Comment

Previous Post Next Post