WAFANYABIASHARA WAASWA KUSAJILI BIASHARA ZAO
Wafanyabiashara wa mifugo wanaojihusisha na masoko ya ndani na nje ya nchi wameaswa kusajili biashara zao ili kurahisisha utendaji kazi kwa ufanisi na usalama zaidi.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Afisa Mwandamizi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Koya Aboubakar, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwa siku nane katika viwanja vya Chinangali.
"Usajili wa biashara si tu unaleta uhalali wa biashara yako kisheria, bali pia unakuwezesha kushiriki katika fursa mbalimbali za kibiashara ndani na nje ya nchi…"
Twaha Abdalah, mmoja wa wananchi waliofanikiwa kusajili biashara yake kupitia maonyesho hayo, ameeleza kuridhishwa na huduma waliyoipata.
"Nilikuja hapa bila kujua kama nitasajili biashara kwa siku moja. Lakini huduma imenipendeza sana, kila kitu ni haraka na bila usumbufu..."
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alifungua rasmi maonyesho hayo na kuwataka wananchi wa Dodoma na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
