WATUMISHI WA BODI YA MAZIWA WAMETAKIWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Serikali kupitia wizara ya Mifugo na uvuvi imewataka watumishi wa Bodi ya maziwa nchini Kutoa huduma kwa kuzingatia misingi ya utawala Bora ili Kupunguza malalamiko kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa kuzingatia misingi mikuu mitatu ikiwemo utaalamu,uaminifu na uwajibikaji katika Kutoa huduma.
Kauli hiyo ya serikali imetoleo leo April 15,2025 jijini Dodoma na Kaimu katibu mkuu wizara ya Mifugo na uvuvi Dkt. Charles Mhina katika kikao kazi ambacho kimewakutanisha watumishi wa Bodi ya maziwa ambapo amesema kila mmoja afanye kazi yake kwa bidii na weledi na kuacha tabia ya kutoa huduma kwa upendeleo.
"Hatupaswi kuwabagua wateja wetu na tunatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi mikuu mitatu ikiwemo utaalamu, uaminifu,na uwajibikaji kwani kufanya hivyo ndiyo misingi Bora ya utoaji huduma'. Amesema.
Sambamba na hayo amewakumbusha watumishi wa Bodi ya maziwa kuzingatia miiko na utunzaji wa Siri za serikali pamoja na kuongeza ari ya utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
"kutunza siri za serikali pamoja na nyaraka za Serikali ni jambo la msingi sana kwa maslahi mapana ya Taifa". Amesisitiza
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Prof. George Msalya amesema kutokana na maziwa kuwa ni chakula Bora kwa Afya ya Binadamu, Bodi ipo Kwenye mchakato wa kuanzisha baa (BAR) za Maziwa nchi nzima ili wananchi wapate huduma katika bar hizo.
"Tumeandaa mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabia nchi kwa lengo la kuelimisha umma kuendelea kunywa maziwa na katika mradi huo tumeandaa Bar za maziwa ili watu wapate sehemu za kukutana maana Kuna watu ambao hawapendi kukaa kwenye bar za vinywaji vingine". Amesema.
Bodi ya maziwa Tanzania imeundwa na Sheria ya maziwa Na.8 sura ya 262 ya Mwaka 2004 Kwa dhamira ya kukuza na kuendeleza tasnia ya maziwa iliyo endelevu na yenye ushindani kwa kuwaratibu wadau, Kwa Kutoa huduma za udhibiti na ushauri Kwa ufanisi na hivyo kuchangia maisha na uchumi wa Taifa.



