WATENDAJI WA SEKTA YA NISHATI TOWENI HUDUMA BORA KWA WANANCHI- DKT. BITEKO
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko amewataka watendaji wa sekta ya nishati nchini kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Biteko ameeleza hayo leo Aprili 9, 2025 jijini Dodoma katika uzinduzi wa Taarifa za Maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2023/24 ambapo amesema wananchi wapewe majibu ya haraka na ya haki kwani wananchi wanahitaji huduma.
"taarifa hii imeonesha bado tuna kazi kubwa ya kufanya. Tunachotaka ni watanzania kupata huduma iliyo bora na hiyo itasaidia kutokuwa na malalamiko ya upatikanaji wa huduma kutoka kwa wananchi,” amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme, mafuta na gesi asilia bado sekta inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwepo mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira, upungufu na uchakavu wa miundombinu.
Ametaja changamoto zingine ni za rasilimali fedha kwa ajili ya uwekezaji na za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hata hivyo, ili kuondokana na changamoto hizo amesema , Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuhakikisha inaboresha, inaimarisha, inarahisisha na inawezesha upatikanaji wa nishati safi kwa Watanzania wote.
“ Namshukuru sana na kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya nishati. Chini ya uongozi wake, tumeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta hii ikiwemo ukamilishwaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na kielelezo ambayo imeongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, upatikanaji wa bidhaa za petroli, pamoja na ongezeko kubwa la matumizi ya gesi asilia hususani kwenye magari,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi EWURA, Prof. Mark Mwandosya ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa inaoendelea kuufanya katika sekta ya nishati.
“ Hii miradi mikubwa hasa ya umeme mfano Bwala la Julius Nyerere inachukua muda mrefu hadi kukamilika kwake hivyo ni kiashiria kwamba tuanze sasa kutekeleza miradi mingine ili baada ya miaka kadhaa tusipate changamoto ya umeme,” amesema Prof. Mwandosya.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), Dkt. James Andilile amesema kuwa uzinduzi wa taarifa hizo ni takwa la kisheria na tayari wameshafanya hivyo kwa upande wa sekta ya maji.
Amesema katika sekta ndogo ya umeme hadi kufikia Juni 2023/2024 uzalishaji wa umeme ulikuwa megawati 2,411 na sasa umefikia megawati 4,032.
“Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme huduma imeimarika na sasa changamoto iliyokuwepo imeondolewa. Kuhusu gharama za bei ya umeme kutokana na uwekezaji katika miundombinu hali ya fedha TANESCO imeendelea kuimarika na mwaka wa tatu mfululizo imetengeneza faida kutokana na usimamizi wa Serikali wa kuondokana na mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme,” amesema Dkt. Andilile
Ameongeza kuwa katika sekta ya mafuta hadi kuishia Juni 2023/2024 vituo vya mafuta vilikuwa 2,361 sawa na ongezeko la asilimia 10, kukiwa na vituo 480 vijijini sawa na ongezeko la asilimia 12. Pia, kuhusu gesi asilia amesema katika mwaka 2020/2023 vyombo vya moto vilivyokuwa vinatumia gesi asilia vilikuwa 7,000 na kufikia Machi mwaka huu vimefikia 15,000 ikiwa ni sawa na asilimia 49.




