VIONGOZI UWT VUNJENI MAKUNDI KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA NA UCHAGUZI MKUU 2025-DKT. NCHIMBI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi awetaka viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kutokubali kununuliwa ili kuipa heshima CCM huku akiwasisitiza kuvunja makundi hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Balozi Dkt. Nchimbi ameeleza kuwa Umoja na mshikamano wa viongozi wa Jumuiya ya UWT utachangia ushindi wa kishindo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Dkt. Nchimbi Ameyasema hayo leo Agosti 2,2024 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Semina ya Wajumbe wa Baraza Kuu la UWT yaliyofanyika katika Ukumbi wa NEC.
“UWT ni miongoni mwa Jumuiya zinazotegemewa kukipa Chama chetu ushindi wa kishindo,hivyo tunapoelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwezi Novemba mwaka huu ninawataka muvunje makundi ili kuwa na mshikamano wa kuipeperusha vyema bendera ya Chama chetu”
Balozi Dkt Nchimbi amewataka viongozi wa UWT kuendelea kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ngazi ya vijiji mpaka Mkoa ili kukutana na wananchi na kuwaelezea Kazi nzuri inauofanywa na Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
Kwa upande wake Katibu mkuu wa UWT Suzan Kunambi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajumbe wa baraza.
Amesema wajumbe hao tayari walishapatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo Matumizi ya takwimu za sensa ya watu na makazi, uchaguzi wa Serikali za mitaa na mafunzo ya uongozi na maadili.
"Leo hii wajumbe hawa watapata mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la malezi na makuzi,". amesema