WAZAZI TIMIZENI WAJIBU WENU WA MALEZI BORA KWA WATOTO WENU-MONGELLA
Serikali imewataka wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kutimiza wajibu wao wa malezi bora kwa watoto wao ili watoto wafahamu mema na mabaya.
Akizungumza katika kongamano la maombi ya ukombozi wa Taifa leo juni 15.202 jijini Dodoma, Mkuu wa wilaya ya Chemba Gerald Mongella amesema wazazi pamoja na walezi wameahidiwa ufalme wa Mungu kutokana na matendo yao lakini watoto wamehaidiwa ufalme huo kutokana na utoto wao, hivyo wazazi na walezi hawapaswi kunya’ganya mtoto haki na fursa aliyoahidiwa na mwenyezi Mungu.
“Watoto si wa kunyanyaswa bali tujitahidi kuwapa baraka zetu kwani kwasasa tumeingiliwa na huu utandawazi hasa janga la ushoga, usagaji, ubakaji na kadhalika na hili jambo ni lazima tujikusanye wote tuanze kupambana nalo,”. Amesema
Sambamba na hayo Mongella amewasisitiza watanzania kuhakikisha wanapambana sana kuzuia unyanyasaji unaomtesa mtoto kwa sababu kitaalamu inaonyesha mtoto akipata unyanyasaji huo ni mara chache sana kukaa sawa kiakili.
"Mara nyingi sana mtoto anapofanyiwa vitendo viovu huwa ina waathiri kisaikolojia na kuwapelekea kwenda kuwa binadamu wasiofaa". Amesema
Ameongeza kuwa Timotheo 2:3 inaeleza jinsi mwisho wa dunia ulivyokaribia kwani yale mengi yaliyotajwa ndiyo yanatokea katika ulimwengu wa sasa hivyo watumishi, wazazi na walezi wanapaswa kupambana usiku na mchana kuhakikisha vita hiyo wanaishinda.
Pia Mongella amesisitiza haki za watoto zilindwe pamoja na kucheza salama, elimu na wajibu wa kupewa upendo pamoja na kuhimiza wazazi pamoja na walezi kuwa na moyo wa kutoa taarifa za matendo wanayofanyiwa watoto sambamba na Kutoa taarifa za viashiria katika vyombo vya sheria ili kukinga matendo ya uovu.
Kwa upande wake Askofu wa kanisa la G.F.C Malaki Solo amesema Taifa lina viongozi wazuri hivyo linapaswa kubadilika kwani serikali ina maadili ya watumishi wake hivyo mchungaji au askofu asipokemea janga la ushoga na usagaji hapaswi kuchunga kondoo wa bwana.
Amesema viongozi wa dini katika mkoa wa Dodoma wamefanya vyema kukusanyika na kuomba katika makao makuu ya nchi kwani mkoa huo umebeba roho nyingi za watu wa makabila na mataifa tofauti.
“Kitabu kile cha Matayo 16:18 inasema nitalijenga kanisa langu wala milango ya kuzimu haitalishinda, kwaio tupo mahali hapa tunajua kwamba kanisa haliwezi kushindwa na kuanzia hapa tunaanza kuwasha moto na jambo hili liwe ni taarifa kwa nchi nzima,”. Amesema
Solo amesema ajenda hiyo ya kitaifa linapaswa liangaliwe na kwa muelekeo mtambuka iweze kukomesha, kukwamisha na pia kuendeleza kupaza sauti kwa wazazi, watoto na vijana kuepuka na kulilinda taifa kuwa na maadili mema.
Pia amesisitiza serikali iendelee kupinga maombi ya kusajili ushoga Tanzania ili kulinda masilahi ya taifa, utamaduni, maisha ya watoto pamoja na hatima ya wasomi wa Tanzania.
Kongamano la maombi ya ukombozi wa Taifa lengo lake ni kumuomba Mungu kukomboa Taifa dhidi ya tatizo la ushoga,ulawiti na usagaji ambalo limewakutanisha watumishi wa Mungu pamoja na vikindi vya kusifu na kuabudu vikiwepo kuwasaidia na kuwaombea wenye shida mbalimbali.