UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA UTAZINGATIA "4R" ZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN-DKT. DUGANGE
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt.Festo Dugange amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utazingatia "4 R"za Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwezesha kila chama kipate nafasi sawa.
Dkt.Dugange ameyasema hay oleo Jijini Dodoma , wakati akifungua kikao cha kupitia rasimu za kanuni za uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unao tarajia kufanyika mwaka huu.
Dkt.Dugange alizitaja rasimu za kanuni zilizoandaliwa kuwa ni Rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za Mwaka, 2024.
Rasimu hizo ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za Mwaka, 2024,uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji za Mwaka, 2024 na Rasimu ya mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo za Mwaka, 2024.
Baadhi ya viongozi wa dini akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Askofu Dk.Israel Gabriel ameipongeza serikali kwa hatua ya ushirikishwaji unaodhihirisha dhamira njema iliyonayo katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa sura namba 287 na sheria ya serikali za mitaa sura namba 288,uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2019 na uchaguzi unaofuata unafanyika mwaka huu 2024.