WATAALAMU WA VINASABA TUMIENI TEKNOLOJIA,WELEDI UWE KIPAUMBELE KWENYE MAJUKUMU YENU: DKT. JINGU


WATAALAMU WA VINASABA TUMIENI TEKNOLOJIA,WELEDI UWE KIPAUMBELE KWENYE MAJUKUMU YENU-DKT. JINGU

Na,Mwandishi wetu-Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu, ametoa rai kwa kamati ya kitaalamu wanaofanya uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu kuzingatia matumizi ya teknolojia huku wakizingatia weledi na kufuata maadili ya kazi  ili kuepuka madhara au migogoro inayoweza kujitokeza.

Dkt. Jingu amesema hayo leo 6 Mei, 2024 jijini Dodoma wakati akizindua  Kamati ya kitaalamu ya Vinasaba vya Binadamu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Vinasaba vya Binadamu Sura ya 73 inayo ongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu.

Katibu Mkuu Dkt. Jingu amesema serikali ina imani na kamati hiyo kwani itasaidia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutimiza wajibu wake kwa nchi na Serikali na kuendeleza mahusiano mema na Taasisi ambazo zina majukumu yanayoshabihiana.

“Ni matumani yangu kuwa kamati tunayoizindua hii leo itasaidia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutimiza wajibu wake kwa nchi na Serikali, lakini pia itaendeleza mahusiano mema ya kiutendaji kati ya Mamlaka hii na taasisi ambazo zina majukumu yanayoshabihiana”. Amesema Dkt Jingu.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa, Masuala ya Vinasaba yana mambo mengi ambayo yanaweza kuisaidia jamii, lakini pia yanahitaji kiwango kikubwa cha kimaadili na kiusimamizi, hivyo amewataka wataalam  kufanya kazi kwa weledi na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya vinasaba kwa kuwa dunia inabadilika kwa haraka kila siku.

Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, ametaja majukumu ya msingi yanayofanywa na Mamlaka ikiwemo sheria ya Udhibiti Matumizi ya Vinasaba vya Binadamu sura ya 73.

“Chini ya sheria hii Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inafanya kazi ya kusajiri na kukagua wadau wa maabara zinazojishughulisha na uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu nchini kwa lengo la kuweza kudhibiti matumizi mabaya ya taarifa za vinasaba, kwa mujibu wa sheria hii Mamlaka pia imepewa jukumu la kutoa vibali vya kufanya utafiti wa suala linalohusisha Vinasaba vya Binadamu”. Amesema Dkt. Mafumiko.

Naye, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Tumaini Nagu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ameahidi kupokea maelekezo yote yaliyoainishwa kwenye kamati hiyo na kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.

“Kwa niaba ya wajumbe wenzangu wote wa kamati hii ya kitaalamu ya vinasaba tunasema tumepokea maelekezo yote, kuhusu unyeti wa kazi hii, lakini pia kuhusu mabadiliko ya teknolojia ambayo yanaenda kwa kasi sana na vilevile maelekezo kuhusu masuala ya ustawi wa jamii na usalama wa watu wenyewe na usalama wa nchi na kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wakati na inazingatiwa. Niseme tu kuwa tumepokea na sisi tunaahidi tutatimiza kazi yetu kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo”. Amesema Dkt. Nagu.






Post a Comment

Previous Post Next Post