DENI LA TOZO KWA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI LAFIKIA SHILLINGI BILLIONI 4.6



DENI LA TOZO KWA MAMLAKA ZA MAJI NCHINI LAFIKIA SHILLINGI BILLIONI 4.6

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

SERIKALI kupitia wizara ya Maji imezitaka Mamlaka za Maji zote  zinazodaiwa kuwasilisha deni la tozo zake ili kuiwezesha EWURA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 

hii nikutokana na deni la Tozo kwa Mamlaka za Maji kufikia takribani Shilingi Bilioni 4.6. 

Akizindua Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2022/23 ambayo ni ya 15 kutolewa na EWURA, Mhandisi Mwajuma Waziri  Katibu Mkuu wa wizara ya Maji  amezitaka mamlaka hizo  zinazodaiwa ankara za maji  zilipe madeni yake mapema ili kuziwezesha kujiendesha na kuweza kutoa huduma kwa ufanisi.

"Kwa Mamlaka za Maji ambazo utendaji wake hauridhishi niseme wazi hatutasita kuzichukulia hatua, nafahamu kuwa baadhi zinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za bei ya maji kuwa chini ikilinganishwa na gharama za uendeshaji". Amesema.

Aidha,Katibu mkuu huyo amewasisitiza watendaji wanaohusika katika usimamizi wa miradi ya Maji nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria.

"Kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hii, wahakikishe wanaikamilisha kwa wakati'tunafahamu moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya maji nchini ni pamoja na kuchelewa kutekelezwa kwa miradi,sitovumilia kuona hili likijitokeza katika miradi hii mikubwa na yenye maslahi makubwa  kwa taifa"Amesisitiza 

Licha ya hayo,ameziagiza Mamlaka za Maji kushirikiana na  Halmashauri zote za Wilaya kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua katika ngazi zote hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

"Tumejionea mvua hizi katika baadhi yua maeneo zimeleta madhara makubwa, hivyo basi,endapo tutavuna maji haya tutapunguza kama siyo kuondoa kabisa athari zake na pia  kutaiwezesha nchi yetu na wananchi kuwa na akiba ya maji ambayo yatatusaidia kipindi cha ukame". Amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile amesema taarifa iliyozinduliwa leo ni ya 15 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo miaka 18 iliyopita na inahusisha uchambuzi wa utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 85 zikiwemo; mamlaka 25 za mikoa, saba (7) za miradi ya kitaifa, 47 za wilaya na Sita (6) za miji midogo.

Dkt.Andilile amesema  Utendaji wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira umeendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022/23, Mamlaka za Maji 78 kati ya 85 zilipata alama kuanzia wastani hadi vizuri sana katika utendaji wa ujumla ikilinganishwa na mamlaka 77 kati ya 90 kwa mwaka 2021/22.

Ameyataja Maeneo yaliyoimarika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2021/22 kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha maji yaliyozalishwa kutoka mita za ujazo milioni 393 hadi 400 sawa na asilimia 1.8 , kuimarika kwa uwiano kati ya watumishi na wateja kutoka 4.2 hadi 3.8 kwa kila wateja 1000 , kuimarika kwa Uwiano wa maunganisho yaliyofungwa dira za maji kufikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 90 ,kuongezeka kwa kiwango cha ubora wa maji yanayosambazwa kwa wateja kutoka asilimia 91 hadi 94;

Maeneo mengine ni kuongezeka kwa wateja wa maji wa majisafi kutoka kutoka 1,385,485 hadi 1,532,362 sawa na asilimia 11 na kuongezeka kwa wateja wa mtandao wa uondoaji majitaka kutoka wateja 55,996 hadi wateja 56,899 sawa na asilimia 16.

“Nafahamu kuwa mafanikio hayo hayakuja bure. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wewe Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi wako mahiri wa sekta ya maji kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na kuimarisha ustawi wa watanzania wote, kwani maji ni UHAI.,” amesema Dkt. Andilile

Uzinduzi huo umekwenda sambamba na utoaji wa tuzo mbalimbali Kwa Mamlaka zilizofanya vizuri huku zikigawanywa katika makundi Matatu tofauti kulingana na idadi ya wateja inayowahudumia ambapo kundi la kwanza ni Mamlaka za maji zenye wateja chini ya 5000, kundi la pili ni mamlaka za maji zenye wateja chini kati ya 5000 na 20,000 na kundi la Tatu ni mamlaka za maji zenye wateja zaidi ya 20,000.

Post a Comment

Previous Post Next Post