ASILIMIA 51 YA WATOTO WA KIKE WENYE UMRI WA MIEZI 24 HADI 59 WAPO KWENYE MWELEKEO MZURI WA UKUAJI HUKU WATOTO WA KIUME UMRI KAMA HUO NI ASILIMIA 44
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Kwa mujibu wa sayansi ya malezi na makuzi inaonesha kuwa Asilimia 47 ya watoto wenye miezi 24 hadi 59 ndiyo wanaolelewa katika mwelekeo sahihi wa kukua kufikia utimilifu wake.
Kati ya hao asilimia ya watoto walio katika mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu inapungua kadri umri unavyoongezeka kutoka asilimia 36 kwa watoto wa miezi 24 -35 mpaka asilimia 58 kwa watoto wa umri wa miezi 48 -59.
Naibu Katibu mkuu wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia wanawake na Makundi Maalumu Wakili Amoni Mpanju ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku Moja Cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi,na Maendeleo ya awali ya Mtoto ambapo amesema Asilimia 51 ya watoto wa kike wenye umri wa miezi 24 – 59 wapo kwenye mwelekeo sahihi wa ukuaji kiafya, kujifunza na katika ustawi wa kisaikolojia na kijamii,ikilinganishwa na asilimia 44 ya watoto wa kiume wenye umri kama huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi huduma za ustawi wa jamii,ofisi ya Rais TAMISEMI Subisya kabuje amesema serikali inaendelea kutekeleza programu jumuishi ya Taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto katika kuhakikisha watoto wote nchini wanafikia ukuaji timilifu.
"natambua kuwa utafiti huu umekuja kuongeza chachu katika utekelezaji wa shughuli za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwani kila mtaalamu kwa sehemu yake katika utoaji wa huduma anatekeleza shughuli za kusimamia makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa njia moja au nyingine ikiwemo shughuli za Ulinzi na Usalama wa Mtoto, kutoa malezi mbadala kwa watoto waliokosa malezi, utoaji wa elimu kwenye vituo vya malezi ya watoto mchana, utambuzi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, utoaji wahuduma za lishe na chanjo, utoaji wa elimu ya malezi kwa wazazi/walezi juu ya malezi na makuzi ya mtoto". Amesema
Naye Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Mlemba Abassy, ambaye ni mtawimu, amesema kutokana na utafiti kuwa mchache wataendelea kushirikina na TAMISEMI,ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na wadau wengine ili kupata viashiria vingi kuhusiana na malezi, makuzi na maendeleo ya awali mtoto.
"Kama Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF ) tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ya Watoto ikihusisha masuala ya Afya, Lishe, Ulinzi wa Mtoto, Elimu, Malezi na Makuzi, na pia kwa kuwezesha Kikao hiki. Amesema.
Kikao kazi hicho Cha siku Moja kimewakutanisha makatibu tawala wa mikoa, wasaidizi wa makatibu tawala, ustawi wa jamii pamoja na Maafisa lishe na Elimu kwa lengo la kuhakikisha watoto wa kitanzania wanakua katika muelekeo wa kufikia utimilifu wao.