SERIKALI YAWAFUTA MACHOZI WANA MBARALI
Na,Mwandishi wetu- Mbeya
Serikali imekabidhi misaada ya kibinadamu yenye thamani ya shilingi Milioni 23 kwa waathirika wa maafa ya mvua iliyombatana na upepo mkali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja, nyumba 42 kuezuliwa nyumba tatu zikibomoka kuta katika Kata sita jumla waathirika wakiwa ni 198 katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Akizungumza wakati akikabidhi misaada hiyo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga amesema hatua hiyo ni sehemu ya pole za Serikali kwa wananchi na kuunga mkono juhudi zilizofanyika za kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa kutokea ambapo amekabidhi mabati 500, Magodoro 100, na mifuko ya Saruji 200 kwa ajili ya waathirika wa maafa hayo.
Mhe. Ummy ametoa wito kwa wananchi wote kuhakikisha wanatekeleza maelekezo yote yanayotolewa na mamlaka husika ikiwa ni pamoja na kuhama katika maeneo hatarishi na kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo salama.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanaopatwa na maafa mbalimbali wanapata huduma stahiki kama ambavyo mmeona namna ambavyo Serikali inaendelea kushughulikia maafa yaliyototea Hanang na yaliyotokea hapa Mbarali na maeneo mangine kote nchini,”Amesema Mhe. Ummy.
Aidha amemuagiza Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Mbarali kuhakikisha unahamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao hatua itakayosaidia kupatikana kwa hali ya hewa safi na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.
“Nikupongeze wewe binafsi na Kamati za Usimamizi wa Maafa Mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Mbarali kwa jitihada ambazo zimefanyika baada ya maafa haya kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa msaada stahiki kwa wakati pamoja na jitihada za kurejesha hali ambazo zimefanyika na zinaendelea kufanyika,”Amebainisha Mhe. Ummy.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini Bw. Beho Malisa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Juma Homera ameishukuru Serikali kwa msaada huo akisema ni nia njema ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wake wanaishi katika mazingira salama hasa wakati huu wa siku kuu ya Kristmas na mwaka mpya huku akiwahimiza wananchi kuendelea kuiamini Serikali.
“Niwapongeze wana Mbarali kwa kuwa watulivu katika kipindi hiki na Serikali pia kwa kutukimbilia kwetu sisi ni faraja na wananchi wetu sasa watapata kivuli na tupoelekea katika msimu wa siku kuu ya Kritsmas na mwaka mpya basi na wao watasherehekea vizuri kama wenzao,”Ameshukuru Mhe. Malisa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbarali Mhe. Bahati Ndingo amepongeza juhudi za Serikali kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuwashika mkono waathirika wote wa maafa katika Wilaya ya Hanang mkoani Mnayara pamoja na Wilaya ya Mbarali akisema misaada hiyo inarejesha hali za wananchi na kujiona ni sehemu ya jamii.
Akitoa shukrani zake mkazi wa Kijiji cha Wambura, Kitongoji cha Nganga Bi. Melina Mkena ameushukuru uongozi wa Mkoa pamoja na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake na kutoa msaada mara tu baada ya tukio la kuezuliwa kwa nyumba yake akisema wakati tukio hilo linatokea alikuwa akiendelea na shughuli zake za kilimo shambani.
Aidha Mkazi wa Kijiji cha Wambura, Kitongoji cha Nganga Bw. Danke Mangengere ameeleza kwamba pindi maafa hayo yanapotokea husababisha kuyumba kiuchumi, uharibifu wa mali zao pamoja na kusababisha vifo hivyo hatua ya Serikali kuwapelekea misaada ni jambo la faraja kubwa kwao kwani husaidia kupunguza makali ya maisha na kurejesha hali zao.