TSC YAWATAKA WALIMU WAKUU KUTOA ELIMU YA AJIRA MAADILI NA NIDHAMU KWA WALIMU WANAOWASIMAMIA



TSC YAWATAKA WALIMU WAKUU KUTOA ELIMU YA AJIRA MAADILI NA NIDHAMU KWA WALIMU WANAOWASIMAMIA

Na,Mwandishi wetu – Dodoma.

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewataka Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kutoa elimu kwa walimu juu ya Sheria Kanuni na Taratibu mbalimbali za Utumishi wa Walimu ili kuongeza ufanizi katika utendaji wa kazi.

Agizo hilo limetolewa na Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama Novemba 8, 2023 wakati akiwasilisha mada juu ya Ajira Maadili na Maendeleo ya Walimu katika Mkutano wa tano wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (TAPSHA) unaofanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Swaswa jijini Dodoma.

“Walimu Wakuu mna wajibu wa kuwanisi walimu mnaowasimamia ili kila mwalimu ajue kipi cha kufanya na kipi hakifai kufanywa kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Walimu na Utumishi wa Umma kwa ujumla,” alisema Katibu huyo. 

Aliongeza kuwa, “ninawasisitiza kuweka kipaumbele katika kutoa elimu kwa walimu mnaowasimamia na msisitizo zaidi kwa walimu wa ajira mpya ambao ili wasifenye vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya ualimu.”

Nkwama alifafanua kuwa pamoja na elimu kutolewa, pale inapotokea mwalimu anakiuka maadili ya kazi ni lazima achukuliwe hatua za kinidhamu ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu ni Mamlaka ya kwanza ya Nidhamu kwa walimu. 

Alieleza kuwa Mwalimu Mkuu/Mkuu wa Shule ana mamlaka ya kumchukulia hatua mwalimu kwa makosa mepesi ambapo pale kosa la mwalimu linapothibitika anaweza kutoa adhabu kama onyo, karipio na kulipa fidia.

Hata hivyo, alieleza kuwa pamoja na Sheria kueleza wazi na viongozi hao wa shule kupewa elimu mara kwa mara, wengi wao bado hawachukui hatua za kinidhamu kwa walimu wanaokiuka miiko na maadili ya utumishi wa walimu jambo linalosababisha utovu wa nidhamu na mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya walimu.

“Suala la ninyi viongozi kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu bado mnalionea aibu. Mwalimu anafanya mambo kinyume na maadili lakini Mwalimu Mkuu huchukui hatua kisa unaogopa kuonekana mbaya. Kumbuka ulipewa dhamana hiyo kwa kuwa ulionekana unaweza kumudu majukumu ya uongozi ambapo moja ya hayo ni kumchukulia mwalimu hatua pale inapohitajika,” alisema Mwl. Nkwama.

Mkutano huo wa TAPSHA ulikuwa na Kauli Mbiu isemayo, “Yamewezekana yasiyowezekana katika elimu nchini,” ambapo mgeni rasmi katika ufunguzi alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) alikimwakilisha Waziri wa Nchi katika Ofisi hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb).

Post a Comment

Previous Post Next Post