NI ASILIMIA 53.8 TU YA NGUVU KAZI WANATUMIA HUDUMA RASMI ZA FEDHA NCHINI-DKT. MWAMWAJA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Serikali kupitia wizara ya Fedha na Mipango imekusudia kutekeleza kwa nguvu mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya Fedha wa mwaka 2020/2021/2029/2030 ambapo ifikapo mwaka 2025 takribani Asilimia 80 ya wananchi watakuwa wamepata uelewa wa Masuala ya fedha.
Kutokana na utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 Nchini, ni Asilimia 53.8 tu ya nguvu kazi wanatumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la watanzania ambao hawafaidiki na huduma za Fedha na kupelekea kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zingewawezesha kuchangia katika pato la Taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 15,2023 jijini Dodoma na Dkt. Charles Mwamwaja Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka wizara ya fedha na Mipango wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Madhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ambayo yanatarajiwa kufanyika Jijini Arusha Tarehe 20 na 26 Novemba 2023 katika viwanja vya Shekhe Amri Abeid.
Aidha,Dkt. Mwamwaja amesema lengo la wiki ya huduma za Fedha ni kujenga uelewa na weledi kwa Umma katika matumizi ya sahihi ya huduma za Fedha zinazotolewa ili kujenga Uchumi na kuondoa umaskini
Sambamba na hayo, Dkt. Mwamwaja amesema wiki ya huduma za Fedha unatarajiwa kuwa na matokeo chanya Kwa mtu binafsi,kaya, jamii na Taifa kwa ujumla ili kuongezeka Kwa idadi ya watu wenye kiwango cha ufahamu wa Elimu ya Fedha na maarifa Juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma Rasmi za kifedha.
Madhimisho ya wiki ya huduma za Fedha Kitaifa yamepangwa kufanyika katika viwanja vya sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia tarehe 20 mpaka 26 Novemba 2023 yakiongozwa na kauli mbiu isemayo:"ELIMU YA FEDHA, MSINGI WA MAENDELEO YA KIUCHUMI".
Tags:
Habari