TULIKAMATA WATUHUMIWA 220 KWA KOSA LA KUMILIKI SILAHA KINYUME CHA SHERIA-KAMISHNA MSAIDIZI WA POLISI MLAY
Na,Sifa Lubasi-Dodoma
MKUU wa kitengo cha udhibiti na usajili wa silaha Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bertha Neema Mlay amesema kuwa watuhumiwa 220 walikamatwa kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria na watuhumiwa 17 walikamatwa kwa kumiliki risasi kinyume cha sheria
Alisema hayo juzi wakati wa kikao cha Mtandao wa Polisi wanawake Tanzania na viongozi wa makundi ya wanawake Mkoa wa Dodoma,wakati akitoa mada ya mada ya madhara ya uzagaaji wa silaha ndogo na nyepesi kwa jamii.
“Mwaka jana 2022 baada ya mwezi Septemba. jumla ya watuhumiwa 220 walikamatwa kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria na watuhumiwa 17 walikamatwa kwa kumiliki risasi kinyume cha sheria,” alisema
Alisema kila mwaka Septemba huwa ni mwezi wa msamaha wa kusalimisha silaha zinazomilikiwa jkinyume cha sheria na baada ya Septemba huanza kuwakamata wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa zoezi hilo lilitakiwa kukamilika Septemba 30, lakini limeongezewa muda hadi Oktoba 31,mwaka huu .
“Silaha zina madhara yake zikizagaa mitaani
wanaotumia silaha hizo tunawaona kila leo na wengine tunawajua lakini na tuna vifua vya kutunza siri,” alisema
Alisemakuwa silaha ina faida ikitumika vyema kwa kazi iliyokusudiwa na wakati muafaka ila zikitumika kiholela na kinyume na ilivyokusudiwa inaleta madhara.
Pia sheria ya udhibiti na usajili wa silaha yam waka 2015 na kanuni zake za mwaka 2016 zinaruhusu mtu binafsi, kampuni kumilikishwa silaha, matumizi yaliyoainishwa kwenye sheria hiyo ni kujilinda binafsi, kulinda mazao na kulinda Wanyama, mashindano ya kulenga shabaha.
Silaha inayomilikiwa kinyume na sheria ni silaha haramu.
Alisema kuwa madhara ya uzagaaji wa silaha ni kuongeza uhalifu mauaji, uporaji mali, ujangili, ugaidi, wiziwa mifugo na uharamia baharini.
Ukosefu wa amani, migogoro, matoshio, vita vya wenyewe kwa wenyewe, kurudisha nyuma maendeleo.
Pia huleta ukatili wa kijinsia, kubaka, kulawiti, kilema cha kudumu, kuzorota kiuchumi
Hatua zilizochukuliwa na serilali katika kudhibiti silaha haramu ni kuutangaza mwezi Septemba kuwa wa kurejesha kwa hiari silaha haramu.
Mkuu wa Mtandao wa Polisi WanawakeTanzania,Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Eva Stesheni alisema kuwa madhara ya uzagaaji wa silaha ni makubwa ni wajibu wa kilaanayemiliki silaha kinyume cha utaratibu kuzisalimisha.
Alisema ifikapo Novemba mosi wataanza kuwakamatawote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Akizungumza kwenye mkutano huo, mmoja wa viongozi wanawake kutoka soko la Sabasaba.
Anna James, alitaka mabalozi kuwa na utaratibu wa kuwatambua watu wanaoingia kwenye maeneo yao ili kupunguza uhalifu.
“ Kuna maeneo ukienda lazima mwenyeji atoe taarifa kwa balozi wa nyumba 10, jambo hilo husaidia kujua pale uharifu unapotokea,” alisema
“Kama maadili yameharibika hata wanawake wengi wanauawa kwa kutumia silaha.
Pia alitaka kuangaliwa kwa kisu kama silaha hatari kwa Maisha ya binadamu kwani kimekuwa kikitumika kufanya mauaji katika matukio mengi.