TAFITI ZIKIFANYIKA KWA UMAKINI NCHI NZIMA,ZITAWEZESHA KUGUNDULIKA KWA MADINI YA KIMKAKATI-WAZIRI MAVUMDE


TAFITI ZIKIFANYIKA KWA UMAKINI NCHI NZIMA,ZITAWEZESHA KUGUNDULIKA KWA MADINI YA KIMKAKATI-WAZIRI MAVUMDE

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Wizara ya Madini imedhamiria kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa shughuli za utafiti wa madini nchini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kutoa taarifa sahihi za kijiolojia za madini na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Madini, Mhe Anthony Mavunde ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kikao cha pamoja kati ya wachimbaji wadogo chini ya mwamvuli wa FEMATA ambapo amesema Tafiti zikifanyika kwa umakini zaidi nchi nzima zitawezesha kugundulika kwa madini ya kimkakati pamoja na kupunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini na wachimbaji wakubwa wa madini.

Tukipiga picha nchi nzima,tukawa tunataarifa za madini za nchi nzima tutakuwa tuna utajiri mkubwa kwa sababu tutakuwa na taarifa na tukifanya hivyo tutapunguza migogoro ya wachimbaji wadogo na wachimbaji wakubwa". Amesema Mavumde.

"leo wachimbaji wote wadogo wanakimbilia maeneo ya wachimbaji wakubwa kwa sababu kuna taarifa sahihi za uchimbaji, lengo letu kubwa tutakalokwenda nalo nikuwawezesha Watanzania kufikia uwezo mkubwa wa uchimbaji". Ameongeza Mavumde.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amewataka wachimbaji kuwa wazalendo na siyo kupoteza uzalendo Kwenye utoroshaji wa madini.

"na ukitaka kujua kwamba unapoteza uzalendo huku unatorosha halafu unadai umeme upelekwe migodini, miundombinu ya kwenda migodini iboreshwe na unadai hiki unadai kile serikali ikufanyie na serikali haina shamba na imekupa shamba lake uvune madini uwape Asilimia 7.3, nawakemea watoroshaji wa madini kuacha tabia hiyo ya utoroshaji madini mara Moja". Amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini FEMATA John Bina ameiomba Serikali kutoa msamaha wa kodi wa uingizaji wa mitambo ya Teknolojia zinazotumika Katika Mnyororo wa Thamani wa uchimbaji Mdogo wa madini.

"Kodi kubwa zinazotozwa wakati wa kuingiza vifaa hivi zinachelewesha ukuaji wa uzalishaji wenye tija kwa wachimbaji wadogo, tunaishauri wizara ya Madini na Wizara ya Fedha ziweze kuratibu zoezi hili kwa haraka". Amesema Bina.

Naye Elias Kisome mchimbaji wa zahabu Mkoa wa iringa amesema mikakati ya wizara ya madini ikitekelezwa kwa wakati italeta mafanikio makubwa Katika Sekta ya madini hapa nchini.

"Mkakati wa waziri wa Madini umekuja kwa wakati sahihi na kama tutakwenda hivi kwa kweli Tanzania Wachimbaji na wafanya Biashara wa Madini na Taifa kwa ujumla tutafika mbali zaidi". Amesema Kisome 

Dira ya mikakati ya wizara ya Madini ni vision 2030 "Madini ni Maisha na Utajiri".

Post a Comment

Previous Post Next Post