SERIKALI IMETENGA BILLIONI 4.5 KUWEZESHA MAFUNZO YA MUDA MREFU NA MFUPI KWA WATUMISHI WA TEHAMA

SERIKALI IMETENGA BILLIONI 4.5 KUWEZESHA MAFUNZO YA MUDA MREFU NA MFUPI KWA WATUMISHI WA TEHAMA 

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Ili kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia vijana katika bunifu mbalimbali na jinsi ya kuzikuza, kuzilindana na kuziendeleza, Serikali kupitia Wizara ya Habari mawasiliano na Teknolojia ya habari  imetenga kiasi cha shilingi Bilion 4.5 kuwezesha mafunzo ya muda mrefu  na mfupi kwa watumishi wa  Tehama nchini.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo , Mohammed Khamis Abdulla Katika hafla ya kuwaaga  watumishi 20  kati ya 211 wanaokwenda kusoma nje ya nchi ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa  mradi wa Tanzani ya kidijitali ambapo amesema Serikali imetiliwa mkazo katika Mkakati wa miaka 10 wa Uchumi wa Tanzania ya Kidijitali ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha TEHAMA kwa  kuwa na wataalamu na wabunifu wabobefu kwa ngazi za Kimataifa. 

"ninatoa rai kwa kila aliyepata ufadhili huu; kutumia kikamilifu fursa hii kujifunza kwa bidii na kuwa na uelewa mzuri wa masomo mtakayokuwa mkifundishwa ili mtakaporudi muweze kuleta mabadiliko chanya yatakayo saidia kuboresha utoaji wa huduma za Serikali. Maarifa na ujuzi mtakaopata muweze kuwapatia watumishi wenzenu ili kwa pamoja tuweze kushirikiana na hatimaye kuleta maendeleo ya nchi kwa ujumla". amewasisitiza 

Aidha, Abdulla amesema Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016 inatilia mkazo dhamira ya Serikali  kukuza na kuimarisha mtaji wa Rasilimali watu katika TEHAMA ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na wataalamu ambao wanaendana na mabadiliko ya uchumi wa kidijitali na kusaidia kuendana na nyakati za mapinduzi ya viwanda ambazo zinachangiwa na matumizi ya teknolojia zinazoibuka.

"Teknolojia zinazoibuka ni teknolojia mpya ambazo zinajumuisha pia  teknolojia za zamani zinazosaidia kupata programu mpya. Teknolojia zinazoibuka mara nyingi huchukuliwa kuwa zenye uwezo wa kubadilisha hali ya kiuchumi ya eneo husika kwa kutumda teknolojia ya TEHAMA na ndio inayo chochea maendeleo katika nyakati hizi za mapinduzi ya viwanda". amesema.

Naye, Naibu katibu mkuu  ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi, amewataka watumishi hao waliofanikiwa kupata ufadhili kwa awamu ya kwanza kwenda kuonyesha juhudi na utayari wa kujifunza masuala mbalimbali yatakayotolewa na  kuelezwa wakati wa kipindi chao cha mafunzo yao. 

Mkurugenzi msaidizi idara ya Ulaya na marekani wa Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Africa Mashariki, Gerald Mbwafu amewaasa wanufaika wa mafunzo hayo kuzingatia sheria  na taratibu za nchi  wanazokwenda na  kujiepusha na vitendo viovu  ikiwemo makosa ya kijinai na  madai.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa mafunzo kuendeleza wataalamu wa TEHAMA serikalini Kwenye taaluma zenye uhaba, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Salome Kessy amesema Ufadhili wa Awamu ya Kwanza ya mafunzo ni dola za kimarekani 1,556,307.62 na kati ya wanafunzi hao, wanafunzi wawili watafanya mafunzo kwa muda wa miaka miwili nawaliobaki 18 watafanya mafunzo kwa muda wa mwaka mmoja.

"Mpango huu ulibuniwa kutekelezwa kupitia Mradi wa Tanzania ya kidijitali ambapo watumishi wa umma wapatao 500 watapatiwa mafunzo na Kati ya hao watumishi 50 watapatiwa mafunzo ya muda mrefu na watumishi 450 watapatiwa mafunzo ya muda mfupi kwenye maeneo yaliyobainika". amesema 

Akizungumza kwaniaba ya wanufaika wa mafunzo hayo ,Gregory Katiti ,amesema mafunzo hayo yatawapatia maarifa na ujuzi muhimu wa kiteknolojia ambao utawawezesha kushiriki katika uchumi wa kidigitali na kuchangia katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

"mafunzo haya yatachochea ubunifu na uvumbuzi. Tunapojifunza jinsi ya kutumia teknolojia hizi za kisasa, tunapata fursa ya kuunda masuluhisho mapya na kubadilisha jinsi mambo yanavyofanyika katika nchi yetu na hii italeta mabadiliko chanya kwa maisha ya watu wetu na kuongeza ushindani wa Tanzania katika ngazi ya kimataifa". amesema.

"sisi kama wanufaika tutahakikisha teknolojia hizi zitatumika kutatua changamoto za kitaifa kama vile kuimarisha huduma za afya, kuboresha usalama wa taifa, na kukuza uchumi". ameongeza

Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unalenga kuleta mabadiliko ya Kidijitali kwa kuwezesha maunganisho ya Kijiditali ya Kikanda na Kimataifa ili kuweza kukuza Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy), kuongeza na kubuni ajira zitakazotokana na ubunifu na uwepo wa mazingira wezeshi, uwepo na ukuzaji wa viwanda vidogo vidogo (SMEs na SMMEs), kukuza ustadi wa wataalamu wa ndani ya Serikali na waliopo nje ya Serikali pamoja na kuongeza uwezo wa utoaji wa Huduma za Serikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post