SERIKALI IMEKIRI KWA MWAKA 2020 HADI 2022 JUMLA YA WATOTO 1,988,022 HAWAKUPATA CHANJO YOYOTE NCHINI-WAZIRI UMMY
Na,Saleh Lujuo-Dodoma.
Serikali imekiri kupokea taarifa za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja amethibitika na Ugonjwa wa Polio katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo uchunguzi wa Maabara ulithibitisha mtoto huyo kuwa na maambukizi hayo.
Aidha, kwa mwaka 2020 hadi mwaka 2022, jumla ya watoto 1,988,022 hawakupata chanjo yoyote na kwa kipindi hicho hicho jumla ya watoto 1,595,564 hawakukamilisha ratiba za chanjo mbalimbali za watoto.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo jijini Dodoma na waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akitoa Taarifa Kwa umma Kuhusu Kampeni ya Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio ambapo amesema sababu kubwa ya kujitokeza kwa visa na milipuko ya Magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo ikiwemo ugonjwa wa Polio ni kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 ambao umeleta athari kadhaa kwa afua zingine za afya ikiwemo kuathiri mwitikio wa chanjo mbalimbali nchini.
"Hali hii imepelekea kuanza kujitokeza kwa visa na milipuko ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ambayo yalikuwa yamedhibitiwa ikiwemo ugonjwa wa Surua, Rubella na Polio na Kwa mara ya mwisho, mgonjwa wa Polio nchini aligundulika mwaka 1996 lakini mnamo tarehe 26 Mei 2023 wizara ilipokea taarifa za uwepo wa mtoto mmoja Mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa kuwa mtoto huyu ana maambukizi ya kirusi cha Polio". amesema Ummy.
Aidha,Waziri Ummy ameeleza kuwa kutokana na tishio hilo la ugonjwa wa polio Serikali imeandaa kampeni maalumu ya utoaji wa chanjo dhidi ya polio Kwa watoto ikiwa na Lengo la kuwafikia watoto 3,250,598 waliozaliwa baada ya mwaka 2016 ili kuwakinga dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili kinachoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.
"Pamoja na ukaribu wa kijiografia na mwingiliano mkubwa wa watu uliopo kati ya nchi yetu na nchi zenye mlipuko wa ugonjwa wa Polio hivi sasa, napenda nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa tutakuwa na Kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Polio (nOPV2) kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka nane (8) ambapo Kampeni hii itafanyika kwa siku nne (4) kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba, 2023 katika Mikoa sita (6) inayopakana na nchi zenye mlipuko wa Polio ambayo ni Rukwa, Kagera,Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya". amesema Ummy.
Sambamba na hayo, Waziri Ummy amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Tanzania Bara zitakazohusika na zoezi la utoaji chanjo kusimamia kwa karibu maandalizi na utekelezaji wa kampeni hii kupitia Kamati za Afya ya Msingi ngazi za Mikoa na Wilaya.
"Nawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha upatikanaji wa chanjo, vifaa na mafunzo kwa wataalam watakaohusika katika utoaji wa chanjo". ameelekeza Ummy.
Waziri Ummy ametoa Rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.
Kampeni hiyo maalum ya chanjo ya polio Kwa watoto wenye umri chini ya miaka 8 itafanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba mwaka huu.